Mada za sehemu hiiUhakiki Kazi Za Fasihi AndishiMada 3
Ni mgawanyo, mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Ni jinsi msanii wa kazi ya fasihi alivyoifuma, kuiunda na kuunganisha tukio moja na lingine, sura moja na nyingine, ubeti na ubeti, na hata mstari wa ubeti na mwingine.
-
Muundo wa moja kwa moja/msago Huu ni muundo wa moja kwa moja ambao matukio huelezwa kwa kuanza la mwanzo hadi la mwisho. Kwa mfano, mhusika huzaliwa, hukua, huchumbia au huchumbiwa, huoa au huolewa, huzaa watoto, huzeeka, hufa. Riwaya ya "Kuli" imetumia muundo huu. Katika riwaya tunamwona Rashidi, akizaliwa, akiwa, anaanza kazi, anaoa, anaanza harakati za kudai haki za makuli na mwisho anafungwa.
-
Muundo wa kioo/rejea Huu ni muundo unaotumia mbinu rejeshi ambayo huweza ama kumrudisha nyuma msomaji wa kazi ya fasihi katika mpangilio wa matukio yake au kuipeleka mbele hadhira ya kazi hiyo. Riwaya ya "Zaka la Damu" imetumia muundo huu.
-
Muundo wa rukia Huu ni muundo ambao visa na matukio hurukiana. Katika muundo huu kunakuwa na visa viwili ambavyo hurukiana katika kusimuliwa kwake, na mwisho visa hivi huungana na kujenga kisa kimoja. Mfano Njama.
Mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii huiwasilisha kazi yake kwa jamii. Ni upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hudokeza upekee wa mwandishi.
Kufichua hisia za mwandishi
Mtindo humwezesha msomaji au msikilizaji kuelewa hisia, msimamo, au mtazamo wa mwandishi kuhusu jambo analolizungumzia. Mfano, matumizi ya lugha ya kejeli, ya huzuni au ya furaha yanaweza kuonesha hisia alizonazo mwandishi kuhusu tukio fulani.
Kudokeza hisia na mwamko wa wahusika
Kupitia mtindo, msanii huonesha namna wahusika wanavyohisi au kujibu mazingira yanayowazunguka. Mfano, matumizi ya lugha ya mashairi au misemo ya wahenga yanaweza kuonyesha hali ya busara au hekima kwa mhusika.
Kuonesha mtiririko wa matukio
Mtindo mzuri husaidia kupanga matukio kwa mpangilio unaoeleweka na unaovutia. Hii husaidia msomaji kufuatilia hadithi kwa urahisi na kuelewa uhusiano kati ya matukio mbalimbali ndani ya kazi ya fasihi.
Kuuumba ulimwengu wa msanii
Mtindo humpa msanii uwezo wa kuunda ulimwengu wake wa kisanaa unaoendana na maono yake. Kwa kutumia mitindo mbalimbali kama ucheshi, kejeli, au uchungu, msanii hujenga mazingira yanayoendana na ujumbe anaotaka kuwasilisha. Hii husaidia kuepusha migongano ya moja kwa moja na wasomaji au watazamaji kwa kutumia mbinu za kifasihi kufikisha ujumbe kwa njia ya hekima au kificho.
Kwa mfano, katika riwaya ya "Kusadikika" ambayo imeumbiwa ulimwengu ulioko angani na nchi inayondelea.
Katika mtindo huangaliwa:
- Matumizi ya lugha
- Nafsi zilizotumiwa
- Matumizi ya monolojia (maelezo/masimulizi) na dialojia (majibizano).
- Mbinu ya kutumia tanzu nyingine za fasihi simulizi
- Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi
- Matumizi ya barua n.k.
Wahusika wakuu
Hawa ni wale ambao wanajitokeza kila mara katika kazi za fasihi, hutokea tangu mwanzo hadi mwisho. Wahusika hawa hubeba kiini cha dhamira kuu na maana ya hadithi yote. Vituko, visa na matendo yote hujengwa kuwahusu au kutokana nao. Mara nyingi jambo hili limewafanya wahusika wakuu wa kazi ya fasihi wawe "midomo" ya wasanii, na pia vipaza sauti vya watunzi wa kazi za fasihi. Wahusika wakuu hasa wameelezwa kwa mapana na marefu juu ya maisha na tabia zao ili kuukamilisha unafsi wao.
Wahusika wadogo/wasaidizi
Hawa hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kuukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Hawa husaidia kuijenga dhamira fulani katika kazi ya fasihi na hasa hubeba dhamira ndogo na kwa minajili hiyo huitwa wahusika wadogo ingawa wakati fulani husaidia kujenga na kuikamilisha dhamira kuu.
Wahusika wajenzi
Hawa ni wahusika ambao wamewekwa ili kukamilisha dhamira na maudhui fulani, kuwajenga na kuwakamilisha wahusika wakuu na wasaidizi.
Wahusika wakuu na wadogo huweza kuwekwa katika aina tatu:
Wahusika bapa
Hawa ni wahusika ambao hawabadiliki kitabia wala kimawazo kulingana na mazingira au matukio ya wakati wanayokutana nayo.
Wahusika bapa huweza kugawanywa kwenye makundi mawili:
-
Wahusika bapa – sugu Hawa huwa sugu katika hali zote, kiasi kwamba hata tuwaonapo mahali pengine hali zao ni zile zile, wao ndio huhukumu, hushauri na kuongoza tu na si vinginevyo wanakuwa kama madikteta. Mfano "Bwana Msa" katika riwaya ya "Mzimu wa watu wa kale" ya M.S. Abdulla.
-
Wahusika bapa – vielelezo Hawa pamoja na kutobadilika kwao, hupewa majina aghalabu ya kiishara ambayo humfanya msomaji aelewe tabia na matendo yao. Mfano: "Waziri Majivuno", "Adili", "Utubora" na "Karama" katika kazi za "Shaaban Robert" ni mfano wa wahusika bapa walio, kiasi ambacho anaondoa sehemu zote za sifa za wahusika huyo.
Wahusika duara/mviringo
Matumizi ya misemo na nahau katika kazi za fasihi hushabihiana sana na yale ya methali. Misemo na nahau hutumika kwa madhumuni anuai kama vile kutambulisha mazingira na wakati husika wa kazi hiyo, lakini pia kupamba kazi ya fasihi pamoja na kuitajirisha lugha ya msanii katika kazi yake.
Tamathali za usemi ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia msisitizo, nguvu na maana katika kazi zao, hali kadhalika kuboresha mtindo wa kazi zao. Wakati mwingine huwa na lengo la kupamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha. Kuna aina nyingi za tamathali za usemi kama ifuatavyo:
Tamathali za mafumbo
-
Dhihaka (Sarcasm) Hii ni tamathali ya dharura na ina lengo la kumweka mtu katika hali duni kupita kiasi, lakini kwa mbinu ya mafumbo. Mfano: "Adella alikuwa msichana msafi sana. Ndiyo maana kila mara alipata kupaka mafuta yaliyonukia na kukaribisha nzi walioleta matatizo makubwa."
-
Tafsida (Euphemism) Hii hupunguza ukali wa maneno au utusi katika usemi. Mfano:
- Kujisaidia au kwenda haja badala ya kunya au kukojoa.
- Kuaga dunia badala ya kufa n.k.
-
Kejeli/Shitizai (Irony) Hii imekusudiwa kuleta maana iliyo kinyume na ile iliyokusudiwa ama kinyume na ukweli ulivyo. Lengo lake ni kutaka kuzuia matatizo na migongano pindi itumikapo kwa lengo maalumu la kufundisha na kuais. Mfano:
- Mtu ni mchafu, lakini anaambiwa – "sijamwona mtu msafi kama wewe."
- Mtu ni adui, lakini anambiwa – "wewe ni rafiki mpenzi."
- Mtu ni mweusi kama mkaa – anaitwa cheupe.
-
Kijembe/Kiringo (Innuendo) Huu ni usemi wa mzunguko, ni usemi wa kimafumbo wa kumsema mtu kwa ubaya.
Tamathali za mliganisho
-
Sitiari (Metaphor) Ni tamathali inayolinganisha matendo, vitu au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti bila kutumia viunganishi linganishi. Mfano:
- Maisha ni moshi
- Pesa ni maua
- Penzi upepo
- Misitu ni uhai
-
Tashibiha (Simile) Tamathali inayolinganisha vitu kwa kutumia maneno kama vile mfano wa, kama, mithili ya, sawa na, n.k. Mfano:
- Ana sauti tamu sawa na ya chiriku
- Ana maringo kama twiga
- Ananyata mithili ya kinyonga
- Ana ng'ang'ania kama kupe.
-
Tashihisi (Personification) Tamathali hii huvipa vitu sifa walzonazo binadamu (hupewa uwezo walionao binadamu). Mfano:
- Mvua iliponyesha misitu ilipiga makofi
- Mawimbi yalitabasamu kwa upepo wa kusi.
-
Lakabu Katika tamathali hii uhusiano wa maneno mawili kisarufi hugeuzwa na pengine huwekwa kinyume na taratibu za kisarufi zilivyo. Mfano:
- Baridi kali ilimkaribisha (lakini mtu ndiye mwenye uwezo wa kukaribisha).
- Giza liliwapokea walipokuwa wakiingia pangoni.
Tamathali za msisitizo na nyinginezo
-
Mubaalagha (Hyperbole) Hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na hata sifa zao kwa madhumuni ya kuchekesha au kusisitiza. Mfano:
- Loo! Hebu muangalie mrembo yule! Ana mlima wa kiuno
- Tulimlilia Nyerere hadi kukawa na bahari ya machozi
- Mrembo yule hubeba kila aina ya silaha na huwatia wazimu wanaume wote anaokutana nao.
-
Taashira/Metonumia (Metonymy) Katika tamathali hii jina la sehemu ya kitu kimoja au la kitu kidogo kinachohusiana na kingine kikubwa hutumiwa kuwakilisha kitu kamili. Mfano:
- Jembe huwakilisha mkulima
- Kutabasamu huwakilisha furaha
- Mvi huwakilisha uzee
- Kalamu huwakilisha mwanafunzi/msomi.
-
Majazi Hii ni aina ya sitiari ambayo itajapo sehemu tu ya kitu hapo hapo sehemu hiyo huashiria na kuwakilisha kitu hicho. Mfano:
- Roho – mtu
- Masikini, ajali ile ilipoteza roho tano hapo hapo.
-
Taniaba (Antonomasia) Hii ni tamathali ambayo kwayo jina la mtu binafsi hutumiwa kwa watu wengine wenye tabia, mwenendo, hali au kazi sawa na ya mtu huyo. Mfano:
- Yesu – mkombozi
- Yesu wa kwanza wa Afrika alikuwa Kwame Nkrumah
- Nyerere alikuwa Yesu wa kwanza Tanzania.
-
Tabaini (Antithesis) Hii ni usemi unaosisitiza jambo kwa kutumia maneno ya ukinzani (unyume). Mfano:
- Mwanadamu hupanga, Mungu hupanga
- Amekuwa mrefu si mrefu, mfupi si mfupi ni wa kadiri
- Usimwamini mtu, yu acheka machoni, rohoni ana mabaya.
-
Takriri (Tautology) Hapa yanakuwepo marudio kwenye sentensi au kwenye usemi na lengo ni kusisitiza. Mfano:
- Dunia ni ngumu jamani, ni ngumu
- Haba na hapa hujaza kibaba
-
Mdokezo (Aposiopesis) Hapa msemaji au mwandishi hukatiza maneno au huacha maneno bila kutaja kitu au maneno ambayo kwa kawaida ni wazi na huweza kujazwa kwa ubunifu. Mfano:
- Ally alipokuwa analia alisema…
- Watu wengi huambukizwa ukimwi kwa kushiriki…
-
Tashtiti (Rhetorical Questions) Ni mbinu ya kuuliza maswali kwa jambo ambalo majibu yake yanafahamika. Mfano:
- Asha na uzuri wake amekufa?
- Loo! Asha ametutoka?
- Hatakuwa nasi tena?
-
Nidaa (!) Huu ni msemo unaoonesha kushangazwa na jambo fulani. Msemo huu huambatana na alama ya kushangaa. Mfano:
- Baba ndiye amefariki!
- Ah! Havijawa nimekutoroka!
- Hakika nitakupenda!
-
Mjalizo (Asyndeton) Hapa huwa ni mfuatano tu wa maneno yasiyo na viunganishi vyovyote bali hutengwa kwa alama ya mkato (,). Mfano:
- Nilikaa, nikasubiri, nikachoka
- Nilipanda, nikapalilia, nikavuna, nikauza, nikajenga nyumba.
Mwalimu
Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.
Ingia ili kuuliza