Sonzaschool
Rudi

Sekondari ya Juu · Kidato cha Tano

Kiswahili 1

Uhakiki kazi za fasihi andishi

takriban dakika 4 kusoma

Mada za sehemu hiiUhakiki Kazi Za Fasihi AndishiMada 3

Uhakiki wa kazi za fasihi

Uhakiki ni kazi au kitendo cha kutafakari, kuchambua, na kufafanua kazi ya fasihi ili kuweka bayana maadili na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi. Hivyo mhakiki sharti asome kazi ya fasihi andishi au kusikiliza masimulizi kwa makini ili aweze kuyahakiki.

Mhakiki ni mtu anayejishughulisha na kazi za kisanaa hususan za kifasihi za wasanii asilia. Mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa kazi za kifasihi. Ni jicho la jamii kwani ndiye agunduaye mazuri yaliyomo katika kazi hiyo, hali kadhali mabaya (hatari) yaliyopo katika maandishi hayo kwa jamii husika.

Mhakiki ni bingwa wa kusoma na kuchambua vipengele vya fani na maudhui katika maandishi ya fasihi. Kwa mantiki hiyo mhakiki ni chombo madhubuti cha jamii inayohusika cha kuleta maendeleo katika jamii.

Wajibika wa mhakiki:

  • Kuwa mwaminifu, mkweli, asiyeogopa kuweka wazi ubaya uliomo katika maandishi ya mwandishi asilia, na asiyependelea waandishi Fulani Fulani kwa sababu zisizona maslahi kwa jamii.

Uhakiki wa kazi za fasihi unaambatana na mambo yafuatayo:

  1. Kuisoma kazi ya fasihi kwa makini na kuielewa.
  2. Kuchambua vipengele vya fani na maudhui katika kazi hiyo.
  3. Kueleza ubora na udhaifu wa matumizi ya vipengele vya fani na maudhui katika kazi hiyo.

Dhima za mhakiki:

  1. Kuchambua na kuweka wazi funzolitolewalo na kazi ya fasihi.
  2. Kuchambua na kufafanua taswira (picha za kisanii) zilizotumika katika kazi ya mwandishi.
  3. Kumshauri na kumtia moyo mwandishi ili afanye kazi bora zaidi (hivyo mhakiki pia ni mwalimu wa mwandishi).
  4. Kumwelekeza na kumchochea msomaji kusoma na kupata faida zaidi ya ambayo angeipata pasipo dira ya mhakiki (mhakiki ni mwalimu na daraja kati ya mwandishi na jamii).
  5. Kuhimiza na kushirikisha fikra za kihakiki katika kazi za fasihi.
  6. Kukuza kiwango cha utunzi na usomaji wa kazi za fasihi.
  7. Kutafuta na kuweka sawa nadharia za fasihi teule.
  8. Kuthamini na kuheshimu kazi za waandishi kwa kuzitendea haki.

Vigezo vya uhakiki

Ukweli wa mambo yanayoelezwa:

  • Mhakiki kama hakimu na daraja atajiuliza, je, ni kweli yaliyoelezwa katika kazi hiyo yanatendeka?
  • Kama anahakiki habari kuhusu ubakaji au rushwa, anapaswa kujiuliza: Je ni kweli mambo hayo yapo katika jamii ya Tanzania?

Uhalisia wa watu, mazingira na matukio katika jamii:

  • Hapo mhakiki analinganisha wahusika wa kazi husika na watu halisi ili kuona kama jamii zungumziwa ina watu wanaotenda kama wahusika waliotumika.
  • Mfano: Habari inaeleza kuwa mganga wa kienyeji aliwapaka dawa watoto wakawaona wachawi, mhakiki anaweza kujiuliza kama kweli hilo linaweza kutokea katika jamii husika.

Umuhimu wa kazi hiyo kwa jamii husika lazima uzingatiwe:

  • Jambo linalozungumzwa linaweza kuwa la kweli na linalihalisika lakini lisiwe na umuhimu mkubwa katika jamii kiasi cha kuvuta utayari wa jamii hiyo.

Vigezo vya kupimia vipengele vya maudhui:

  • Dhamira, ujumbe, migogoro, mafunzo, na falsafa.
  • Vigezo vya kupimia vipengele vya fani:
    • Muundo, mtindo, matumizi ya lugha, wahusika, na mandhari.

Mfano wa kupima kazi

Hadithi inayosifu maisha ya vijijini na kuwashauri vijana wasikimbilie mijini, lazima ipimwe kwa kuzingatia ukweli uliopo vijijini. Mhakiki atajiuliza maswali ya dhamira, mafunzo, migogoro, ujumbe na falsafa kama haya:

  • Je, ni kweli kuwa wanavijiji wana maisha bora kuliko mjini?
  • Je, wanavijiji wanahuduma za lazima kama hospitali zenye waganga na dawa?
  • Je, wanavijiji wana maji salama kwa ajili yao, mifugo na mazao yao?
  • Je, mazao ya wanavijiji yananunuliwa kwa fedha taslimu na mapema?
  • Je, wanavijiji hawa bughudhiwi na wezi, waporaji n.k?

Kuhusu kukimbilia mijini:

  • Je kijana anapokimbilia mjini ana uhakika wa kupata kazi?
  • Je, kazi kama kuuza machungwa au karanga mijini ni shughuli inayoweza kumkimu huyo kijana?
  • Je, vijana wasio na kazi mijini hawalazimiki kuiba au kufanya uhalifu mwingine?

Maswali kuhusu ufumbuzi unaopendekezwa na mwandishi:

  • Je, mwandishi anashauri nini licha ya kusema vijana wabaki vijijini?
  • Je, ni mambo gani anayopendekeza mwandishi kuhusu kuinua shughuli za kiuchumi vijijini?
  • Je, suluhu la mwandishi (mapendekezo) linawezekana (ni yakinifu) au ni la kinjozi tu (la kidhanifu)?

Uhakiki wa fani:

  • Je, kazi husika ina muundo gani?
  • Wahusika wamechorwaje?
  • Je, wahusika wanahalisika katika jamii husika?
  • Je, mpangilio wa maneno unavutia wahusika?
  • Matumizi ya tamathali mbali mbali yanatosheleza haja?
  • Misemo na methali zilizotumika zinafaa hapo zilipotumika au zimepachikwa tu?

Mwalimu

Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.

Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.

Ingia ili kuuliza