Mada za sehemu hiiKuchambua chimbuko la Azimio la Arusha na matokeo yake kiuchumi, kisiasa na kiutamaduniMada 4
- Kufafanua falsafa ya Azimio la Arusha
- Kutathmini mifumo na misingi mipya ya kimaadili iliyoanzishwa na Azimio la Arusha
- Kuchambua athari za Azimio la Arusha kiuchumi, kisiasa, kijamii, kimaadili, kiutamaduni na katika uhusiano wa kimataifa
- Kutathmini umuhimu (relevance) wa Azimio la Arusha katika mazingira ya sasa
Azimio la Arusha na Athari Zake
Azimio la Arusha lilikuwa tamko rasmi la Chama cha TANU lililotolewa tarehe 5 Februari 1967 chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tamko hili lilianzisha falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea kama miongozo ya maendeleo ya Tanzania. Uchambuzi wa kina wa athari za Azimio la Arusha unahusisha kuchambua madhara na manufaa yake katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii, kimaadili, kiutamaduni na uhusiano wa kimataifa.
Athari Chanya
Uanzishwaji wa Viwanda vya Serikali
Azimio la Arusha lilikuwa msingi wa sera ya utaifishaji ambayo ilihamisha umiliki wa mashirika makubwa, benki na viwanda kutoka kwa wawekezaji binafsi kwenda serikalini. Lengo lilikuwa kuhakikisha rasilimali na faida zake zinawanufaisha wananchi wote. Katika kipindi hicho, viwanda vya nguo viliianzishwa ili kuchakata pamba na kuzalisha bidhaa za nguo, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Urafiki jijini Dar es Salaam kilichojengwa kwa ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa China. Viwanda vya saruji kama Tanga Cement vilianzishwa ili kusaidia maendeleo ya miundombinu ya taifa.
Viwanda vya sukari vilianzishwa ili kujitosheleza kwa sukari nchini, na viwanda vya bia na vinywaji baridi kama Tanzania Breweries Limited (TBL) vilitaifishwa. Aidha, viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo kama chai, kahawa, tumbaku na korosho viliwekwa chini ya mashirika ya umma baada ya utaifishaji.
Kuongeza Ajira na Ustawi wa Wananchi
Mabadiliko ya kimuundo ya uchumi yalisababisha ongezeko la ajira katika sekta mbalimbali. Baada ya Serikali kutekelezwa sera za utaifishaji na kuanzisha mashirika ya umma pamoja na viwanda vipya, wananchi wengi, hasa vijana, walipata fursa za ajira rasmi nje ya sekta ya kilimo. Hatua hii ilipunguza utegemezi wa ajira katika kilimo pekee na kusaidia kuibuka kwa tabaka jipya la wafanyakazi wa viwandani.
Kuendeleza Sekta ya Kilimo
Kilimo kilikuwa miongoni mwa malengo makuu ya Azimio la Arusha, kwa kuwa kilitambuliwa kama mkombozi wa wanyonge na njia muhimu ya kuliondoa Taifa katika lindi la umaskini. Kupitia Sera ya Vijiji vya Ujamaa, wananchi walihamasishwa kuishi na kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza tija ya uzalishaji wa kilimo. Serikali ilianzisha viwanda vya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao ya ndani.
Kupunguza Pengo la Kiuchumi
Sera ya Ujamaa ilisisitiza umiliki wa pamoja wa rasilimali na udhibiti wa sekta kuu za uchumi, hatua iliyosaidia kuzuia kujitokeza kwa matabaka makubwa kati ya matajiri na maskini. Faida za maendeleo ziligawanywa kwa usawa zaidi, na hakuna kundi dogo linaloweza kujilimbikizia mali kwa gharama ya wananchi wengi.
Athari Hasi
Kushuka kwa Tija ya Viwanda na Mashirika ya Umma
Ingawa sera ya utaifishaji iliokusudiwa kwanzaisha wananchi, utekelezaji wake ulikumbwa na changamoto za usimamizi. Mashirika mengi ya umma hayakuwa na ufanisi wa kibiashara kutokana na urasimu, ukosefu wa utaalamu wa usimamizi, na upungufu wa mitaji. Viwanda vilishindwa kufikia malengo ya uzalishaji kutokana na ukosefu wa teknolojia ya kisasa na motisha ya ushindani.
Kushuka kwa Uzalishaji wa Kilimo
Mfumo wa umiliki wa pamoja ulipunguza motisha ya uzalishaji binafsi, kwani wakulima walihisi kuwa juhudi zao hazingewaletea faida za moja kwa moja. Uhamishaji wa wananchi kutoka maeneo yao ya asili kwenda vijiji vya ujamaa uliwasababishia usumbufu mkubwa na kuvuruga mzunguko wa kawaida wa shughuli za kilimo.
Ukosefu wa Fedha za Kigeni
Baada ya utaifishaji wa mashamba, benki na mashirika yaliyokuwa yakimilikiwa na wageni, Tanzania ilikumbwa na upungufu wa uwekezaji wa kigeni. Upungufu huu uliathiri uzalishaji wa viwandani na kupunguza upatikanaji wa bidhaa muhimu kama mafuta na dawa.
Athari Chanya
Kuimarika kwa Mshikamano na Umoja wa Kitaifa
Azimio la Arusha liliweka mbele maslahi ya Taifa kwa ujumla badala ya kuruhusu makundi madogo kunufaika peke yake. Kanuni ya usawa ilipunguza uwezekano wa migawanyiko ya kikabila, kidini na kitabaka. Hali hii iliimarisha mshikamano wa kitaifa na kupunguza migongano ya kisiasa, ikifanya Tanzania kujulikana kimataifa kama mojawapo ya nchi zenye uthabiti wa kisiasa barani Afrika.
Kuimarika kwa Uadilifu na Maadili ya Viongozi
Mwongozo wa Uongozi uliweka masharti yaliyowazuia viongozi wa chama na serikali kumiliki mali nyingi, kushiriki katika biashara binafsi au kumiliki hisa katika makampuni. Lengo lilikuwa kuzuia viongozi kujilimbikizia utajiri na kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa uaminifu. Hatua hii ilijenga uhusiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi.
Tanzania Kuheshimika Kimataifa
Azimio la Arusha lilionesha dunia kuwa Tanzania ilikuwa Taifa lililojitolea kujenga siasa safi zenye misingi ya maadili, usawa na kuthamini utu wa binadamu. Kupitia misimamo hii, Tanzania ilitambulika kama kinara wa harakati za ukombozi barani Afrika kwa kuunga mkono mapambano ya uhuru katika nchi kama Zimbabwe, Msumbiji, Angola na Afrika Kusini.
Athari Hasi
Kutegemea Chama Badala ya Taasisi Huru za Kisiasa
Katika kipindi hiki, chama kilishika hatamu ya mamlaka kwa kuwa juu ya mihimili mingine ya Serikali. Taasisi muhimu za kitaifa kama Bunge na Mahakama hazikuweza kufanya kazi kwa uhuru kamili, kwa kuwa mara nyingi zilitegemea maamuzi na miongozo ya chama tawala.
Kuongezeka kwa Urasimu Serikalini
Kwa kuwa chama na Serikali vilidhibiti karibu kila nyanja ya maisha ya wananchi, shughuli nyingi za kisiasa na kiuchumi ziliendeshwa kupitia taratibu ndefu za kiserikali. Mfumo huu wa urasimu ulisababisha maamuzi muhimu kucheleweshwa au kushindwa kutekelezwa kwa wakati.
Athari Chanya
Kuimarika kwa Mshikamano wa Kijamii
Kupitia sera za Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha liliweka msisitizo mkubwa katika umoja, usawa na mshikamano wa kijamaa. Kila raia alihimizwa kujiona kuwa sehemu ya familia moja ya Taifa badala ya kujitambulisha kwa misingi ya kikabila, kidini au kitabaka.
Kuongezeka kwa Upatikanaji wa Huduma za Kijamii
Azimio la Arusha lilichochewa upanuzi mkubwa wa huduma za kijamii, hususan katika sekta ya elimu. Shule nyingi za msingi zilijengwa vijijini na watoto wengi walipata fursa ya kupata elimu. Mwaka 1974, Azimio la Musoma lilianzishwa kwa lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi. Kwa mfano, idadi ya shule za msingi iliongezeka kutoka takribani 5,700 mwaka 1974 hadi zaidi ya 10,000 mwaka 1980.
Sekta ya afya iliboreshwa kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati. Kati ya mwaka 1967 na 1980, idadi ya zahanati iliongezeka kutoka 1,312 hadi 2,789.
Kupungua kwa Matabaka ya Kijamii
Kupitia Mwongozo wa Maadili ya Viongozi, viongozi walizuiwa kumiliki mali kubwa au kushiriki katika biashara binafsi. Lengo lilikuwa kuzuia viongozi kujilimbikizia utajiri binafsi na kuzuia kuibuka kwa tabaka dogo la watu wenye mali nyingi.
Athari Hasi
Uhamishaji wa Wananchi kwenda Vijiji vya Ujamaa
Wananchi wengi walilazimishwa kuondoka katika makazi yao ya asili ambako walikuwa wamezoea mazingira na shughuli za uzalishaji. Uhamishaji huu ulisababisha usumbufu mkubwa wa kijamii na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo.
Kupungua kwa Ari ya Kufanya Kazi
Mfumo wa umiliki wa pamoja uliwapunguzia wananchi wengi ari ya kufanya kazi kwa bidii. Wananchi waliona kuwa juhudi zao binafsi hazikuleta manufaa ya moja kwa moja, hali iliyosababisha baadhi ya watu kupunguza bidii.
Athari Chanya
Kuweka Uadilifu wa Viongozi kama Sharti la Msingi
Kupitia Mwongozo wa Maadili kwa Viongozi wa Umma, viongozi wa chama na serikali waliwekewa masharti ya kimaadili yaliyowazuia kumiliki mali kubwa au kuendesha biashara binafsi. Lengo lilikuwa kuondoa mgongano wa maslahi na kuhakikisha viongozi wanabaki kuwa watumishi wa wananchi.
Kujenga Maadili ya Uzalendo na Kujitegemea
Kupitia falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea, wananchi walihamasishwa kuacha utegemezi wa misaada ya nje na kuamini katika nguvu zao wenyewe. Maadili haya yalihusishwa na nidhamu ya kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji binafsi na kujitolea katika shughuli za kijamii.
Kueneza Elimu ya Uraia na Maadili ya Kitaifa
Azimio la Arusha liliweka msisitizo mkubwa katika utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi wote ili waweze kuelewa misingi ya Ujamaa na Kujitegemea. Kupitia vyuo vya siasa na semina za viongozi, wananchi walielimishwa kuhusu wajibu wao kwa Taifa.
Athari Hasi
Kuongezeka kwa Vibaraka wa Kisiasa
Ingawa viongozi walihubiri hadhari kuhusu ujamaa na maisha ya unyenyekevu, baadhi yao waliishi maisha ya anasa na kujilimbikizia mali kinyume na maadili waliyoyatangaza. Tofauti hii kati ya maneno na matendo iliibua hali ya unafiki wa kisiasa.
Kuibuka kwa Mgongano kati ya Kanuni na Uhalisia
Baadhi ya watuwaliendelea kujinufaisha kinyume kabisa na masharti ya Mwongozo wa TANU. Kadiri pengo kati ya walionacho na wasionacho lilivyozidi kuongezeka, wananchi walizidi kupoteza imani katika maadili yaliyokuwa msingi wa Azimio.
Athari Chanya
Kuendeleza Kiswahili
Kupitia sera za TANU na msisitizo wa siasa ya Ujamaa, Kiswahili kilipewa nafasi ya pekee kama lugha ya Taifa na nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano wa kijamii. Matokeo yake, Kiswahili kilienea na kuwa sehemu ya utamaduni wa maisha ya kila siku ya Watanzania.
Kuimarisha Mshikamano wa Kitaifa
Kupitia falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea, wananchi walihimizwa kuacha kujitambulisha kwa misingi finyu ya kikabila na badala yake kujiona kuwa sehemu ya familia moja ya Taifa. Mwelekeo huu uliweka msingi wa utamaduni mpya wa kitaifa.
Kukuza Maadili ya Kijamaa
Wananchi walihamasishwa kuishi kwa misingi ya unyenyekevu, mshikamano na umoja wa kijamaa kama nguzo kuu za maadili ya Taifa. Kupitia mtindo huu wa maisha, mshikamano wa kijamii na udugu vilijengeka.
Athari Hasi
Kuathiri mitindo ya maisha na mila – Baadhi ya mila na desturi za asili zilipuuzwa au kubadilishwa kwa jina la ujamaa na usasa, jambo lililoathiri utambulisho wa kiutamaduni wa baadhi ya jamii.
Mmomonyoko wa baadhi ya maadili – Mabadiliko ya kiuchumi na mwingiliano na tamaduni za kigeni yalichangia kupungua kwa uzito wa baadhi ya maadili ya jadi ya Kitanzania.
Athari za Azimio la Arusha zinaonekana katika maisha ya kila siku ya Watanzania kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili inayotuunganisha bila kujali kabila, pamoja na huduma za jamii kama elimu na afya zinazotolewa na serikali. Kwa mfano, mwanafunzi anayesoma shule ya umma na kupata matibabu katika zahanati ya serikali ananufaika na msingi wa usawa na huduma za jamii ulioimarishwa na Azimio la Arusha, huku dhana ya kujitegemea ikimhimiza kuthamini kazi na kuanzisha miradi midogo ya kujiongezea kipato.
Swali
Azimio la Arusha lililotolewa tarehe gani?
Ingia ili kuwasilisha jibu lako na lihesabiwe katika umahiri wako.
Ingia ili kufanya mazoeziMwalimu
Umekwama? Niulize chochote kuhusu mada hii.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu swali hili.
Ingia ili kuuliza