Sonzaschool
Rudi

Sekondari ya Kawaida · Kidato cha Tatu

Kiswahili

Ufahamu

takriban dakika 3 kusoma

Mada za sehemu hiiUfahamu Na UfupishoMada 2
  1. Ufahamu
  2. Ufupisho

Ufahamu

Ufahamu ni hali ya kulijua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea kwa ufasaha bila kupoteza maana yake ya msingi. Ni kujua na kuelewa jambo na kuweza kulifafanua.

Madhumuni ya kufundisha ufahamu ni kumwezesha mwanafunzi kuelewa mambo mbalimbali kwa njia ya lugha pamoja na kukuza ustadi wake katika kuzungumza, kusoma na kuandika.

Aina za ufahamu

Ufahamu wa kusoma

Ni kuzingatia maana ya neno, sentensi na habari yote. Msomaji lazima aweze kutambua mpangilio wa herufi, maneno na tarakimu na kuzitofautisha.

Upo usomi wa aina mbili:

  1. Kusoma kimya
  2. Kusoma kwa sauti

Kusoma kimya na kwa haraka

Maana

  1. Ni usomaji wa kupitisha macho kwenye maandishi kwa haraka bila kusoma kwa kina.
  2. Lengo ni kupata ujumbe mkuu haraka.

Mambo ya kuzingatia

  1. Kuwa mtulivu na makini
    • Soma kwa utulivu ili kuelewa kuanzia utangulizi hadi hitimisho bila kuruka aya.
  2. Kuelewa maana ya maneno na misemo
    • Tumia kamusi kupata maana ya maneno.
    • Tumia muktadha (mazingira): Tambua maana ya neno kulingana na jinsi lilivyotumika kwenye sentensi.
  3. Kubuni mawazo (wazo kuu)
    • Kila aya huwa na wazo kuu moja.
    • Zingatia mbinu za kujiuliza (aya hii inazungumzia nini?) ili upate kiini cha habari nzima.
  4. Kubaini matumizi mengine ya lugha
    • Tambua matumizi ya:
      • Nahau
      • Methali
      • Misemo
      • Tamathali za semi
      • Ishara au taswira

Mbinu za kujibu maswali kutokana na habari

  1. Soma nakala inayohusika kwa mara ya kwanza ili kupata muhtasari.
  2. Soma maswali yote ili kujua kinachoulizwa.
  3. Rudia kusoma nakala kwa makini, sasa ukitafuta majibu ya maswali.
  4. Tumia kalamu ya risasi kuweka alama kwenye sehemu unazodhani zina jibu.
  5. Jibu maswali kwa ufasaha ukitumia habari uliyoweka alama.

Kusoma kwa sauti

Maana

Usomaji wa maandishi kwa kutamka kwa sauti.

Faida

Humwezesha msomaji:

  1. Kupata ujumbe
  2. Kutamka lafudhi ya Kiswahili vizuri
  3. Kuimarisha ufasaha wa matamshi

Ufahamu wa kusikiliza

Ni ule ambao muhusika anaupata kwa kusikiliza habari fulani. Inawezekana kupata kwa kusimuliwa au kusomewa.

Ili kupata ufahamu kutokana na habari unayosikiliza, lazima msikilizaji azingatie mambo yafuatayo:

  1. Kusikiliza kwa makini ili kuelewa wazo kuu
  2. Kuhusisha mambo muhimu na habari inayosimuliwa
  3. Kujua matamshi ya mzungumzaji
  4. Kubainisha mawazo makuu

Mambo ya kuzingatia katika ufahamu wa kusikiliza

Kubaini mawazo makuu

Msimulizi akizungumza huwa ana ujumbe anaotaka uwafikie watu. Wakati mwingine hupanga ujumbe huo kwa namna nyepesi ili msikilizaji aupate kwa haraka. Mara nyingine huchanganya wazo zaidi ya moja kutoka aya moja lakini mawazo hayo yanakuwa yanahusiana. Ili msikilizaji aweze kubaini wazo kuu, atalazimika kusikiliza kwa makini.

Kubaini maana ya maneno na misemo

Katika habari ambayo mtu anapata katika kusikiliza aghalabu kuna maneno magumu. Hivyo maana ya maneno itapatikana kulingana na matumizi (maana iliyokusudiwa) kama msomaji ameshindwa kupata maana, anashauriwa kutafuta katika kamusi ya Kiswahili.

Kusikiliza kwa utulivu

Ni wajibu wa msikilizaji kusikiliza kwa utulivu maelezo ya msomaji. Mbinu hiyo itamwezesha kuelekeza fikra zake kwenye maelezo yanayotolewa na hivyo kuweza kuelewa mada vizuri pamoja na maswali, kwa sababu kuna wengine hawamudu vizuri matamshi sahihi ya Kiswahili.

Mfano:

  • raha – laha
  • Fedha – feza

Kujibu kwa ufupi

Baada ya kubaini majibu/jibu la maswali/swali unatakiwa kujibu kwa kutumia maelezo machache tu. Maelezo hayo sharti yawe tu yanahusiana na kipengele kinacholengwa na swali.

Mwalimu

Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.

Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.

Ingia ili kuuliza