Sonzaschool
Rudi

Sekondari ya Kawaida · Kidato cha Nne

Kiswahili

Uandishi wa risala

takriban dakika 3 kusoma

Mada za sehemu hiiUandishiMada 5

Uandishi wa Risala

Maana ya Risala

  1. Risala ni hotuba fupi iliyoandikwa na kusomwa mbele ya hadhira kwa niaba ya kundi fulani.
  2. Lengo lake ni kutoa taarifa, kueleza mafanikio, matatizo au kutoa msimamo wa kundi hilo kwa mgeni rasmi au kiongozi.

Sifa za Risala Nzuri

  1. Huandikwa kwa lugha fasaha, rasmi na ya kuvutia.

  2. Inakuwa na mtiririko mzuri wa hoja (kimantiki).

  3. Msomaji wa risala lazima awe na sauti ya kueleweka, atumie lafudhi sahihi, na azingatie alama za uandishi kama vile:

    • Vituo sahihi
    • Uwekaji wa mkazo
    • Uchangamfu na heshima

Muundo wa Risala

Mwanzo

  1. Kichwa cha risala: Huandikwa kwa herufi kubwa na kupigiwa msitari.
  2. Salamu na utambulisho wa hadhira, mfano:
    "Ndugu mgeni rasmi, waheshimiwa wageni waalikwa, walimu, wazazi na wanafunzi..."

Kiini

Sehemu ya maelezo ya msingi kuhusu:

  • Historia fupi ya taasisi au kundi
  • Mafanikio yaliyopatikana
  • Changamoto zilizopo
  • Matarajio kwa siku zijazo

Hitimisho

  1. Shukrani kwa mgeni rasmi na hadhira.

  2. Wito au ombi kwa kiongozi husika.

  3. Kauli ya kumalizia yenye heshima na matumaini, mfano:

    • "Tunatumaini utayazingatia maombi yetu."
    • "Asante kwa kutusikiliza, Mungu akubariki."

Mfano wa Risala

RISALA YA UONGOZI WA SHULE YA SEKONDARI CHANIKA KWA MHESHIMIWA JUMANNE MAGEMBE, WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI (MB), KATIKA SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA MITATU YA SHULE HII – TAREHE 26.01.2008

Ndugu mgeni rasmi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MB),
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule,
Ndugu walimu, wanafunzi, wazazi na wageni waalikwa,
Kwa niaba ya uongozi mzima wa shule ya Sekondari Chanika, tunayo furaha kubwa kuwakaribisha katika shule yetu ili muweze kushuhudia shughuli mbalimbali za kitaaluma na maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu. Karibuni sana.

Ndugu mgeni rasmi, shule hii ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 800, walimu 12, na wafanyakazi wasio waalimu 8. Kwa sasa, tuna wanafunzi 2000, walimu 30 na wafanyakazi 10. Mafanikio ya shule ni mengi:

  1. Tumekuwa kinara katika matokeo ya kidato cha pili wilaya ya Chalinze.
  2. Tumevuta maji ya bomba kwa matumizi ya shule.
  3. Tuna mgahawa wa shule unaosaidia mapato na huduma za chakula.
  4. Tumefanikisha ujenzi wa zahanati inayohudumia wanafunzi na wakazi wa jirani.

Hata hivyo, tunakabiliwa na changamoto mbalimbali:

  1. Upungufu wa walimu wa Fizikia, Baiolojia, Kemia na Biashara.
  2. Ukosefu wa ukumbi mkubwa wa mikutano.
  3. Kukosa gari la shule kwa shughuli mbalimbali.

Mpaka sasa, tumekusanya milioni 25 kwa ajili ya ukumbi kutoka kwa wazazi, wadau na mapato ya shule. Tunaomba msaada wa serikali kufanikisha lengo letu.

Tunaiomba serikali pia ituwezeshe kupata gari la shule — hata kama ni kwa mkopo.

Ndugu mgeni rasmi, tunakuomba uyazingatia maombi yetu. Tunakushukuru kwa kuitikia wito wetu na kufika hapa.
Asante kwa kutusikiliza. Mungu akubariki.

Mwalimu

Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.

Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.

Ingia ili kuuliza