Sonzaschool
Rudi

Sekondari ya Juu · Kidato cha Tano

Kiswahili 1

Tafsiri

takriban dakika 8 kusoma

Mada za sehemu hiiTafsiri Na UkalimaniMada 2
  1. Tafsiri
  2. Ukalimani

Maana ya tafsiri

Tafsiri ni taaluma inayojihusisha na uhawilishaji wa mawazo au ujumbe ulio katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kusudi maalum.

Dhana za msingi katika tafsiri

  1. Fasili: Ni kufafanua maana ya neno kwa kina.

  2. Kurudufu: Ni kunakili alama au kitu kama kilivyo.

    • Kwa hiyo, urudufu unaweza kuitwa ni unakili.
    • Kwa mujibu wa TUKI (2013), kunakili ni kufuatisha au kutoa kivuli cha mchoro au maandishi kama yalivyo.
  3. Ukafsiri: Ni mchakato wa kitendo cha kukafsiri.

    • Kukafsiri ni kuhawilisha ujumbe kutoka matini andishi kwenda mazungumzo au kutoka mazungumzo kwenda katika maandishi kutoka lugha chasili hadi lugha lengwa, kwa kuzingatia muktadha, isimu na utamaduni wa lugha zinazohusika.
    • Mfano mzuri ni sinema ambazo wahusika wake wanakuwa wanaongea lakini maneno yake yanaandikwa katika runinga chini.
  4. Matini: Ni kifungu cha maneno kilichoandikwa ambacho kimebeba maana au ujumbe fulani.

  5. Matini chanzi: Ni matini inayotafsiriwa kwenda lugha nyingine.

  6. Matini mlengwa: Ni matini iliyotafsiriwa katika lugha lengwa.

  7. Lugha chanzi: Ni lugha iliyotumiwa katika mchakato wa kuandaa matini chanzi.

  8. Lugha lengwa: Ni lugha inayotumiwa katika mchakato wa kuunda matini lengwa.

  9. Mfasiri: Mtu mwenye taaluma au tajiriba ya kutafsiri na ambaye amejikita katika shughuli hizo. Pia lazima awe mjuzi wa lugha zisizopungua mbili.

  10. Nduni za mfasiri kabambe au jamali

Zifuatazo ni baadhi ya sifa au nduni za mfasiri jamali:

  1. Awe mwenye taaluma na ujuzi wa tafsiri mfano awe amesomea kozi ya taaluma ya tafsiri au amepitia mafunzo fulani,
  2. Awe na utashi wa kuibua hisia sawa kwa wapokezi wa ujumbe.
  3. Awe na tajiriba katika taaluma zingine mfano isimu jamii na isimu ethnolojia.
  4. Awe mzawa au mbobevu wa tamaduni mbalimbali. Mwenye kipaji au taaluma ya uhariri, uandishi, na uhakiki wa matini mbalimbali.
  5. Awe na stadi za uhakiki matini.
  6. Awe na maarifa au ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano yaani (TEHAMA)
  7. Awe na tajiriba kubwa ya usomaji wa aina mbalimbali za tafsiri.
  8. Awe na tabia yakushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.

Dhima za tafsiri

Tafsiri ina majukumu lukuki ndani ya jamii hususani katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia. Baadhi ya dhima za tafsiri ni kama ifuatavyo:

  1. Kueneza Utamaduni wa Jamii ya Lugha Chasili: Tafsiri husaidia kueneza utamaduni wa jamii fulani kwa kutafsiri kazi za kifasihi na kitaaluma. Kwa mfano, tamthilia ya Nitaoa Nikipenda ilitungwa kwa Kikuyu, lakini ilipotafsiriwa kwa Kiingereza I Will Marry When I Want, iliwezesha wasomi wengi kuelewa mila na desturi za jamii ya Wakikuyu.
  2. Kutambua Historia ya Jamii Husika: Tafsiri inatoa nafasi ya kutambua historia ya jamii kwa kuleta kazi za zamani zilizoandikwa kwa lugha ya asili. Mfano, tamthilia ya Mfalme Edipode iliyoandikwa kwa Kigiriki, ilitafsiriwa kwa Kiingereza na hatimaye Kiswahili, hivyo kurahisisha ufahamu wa historia ya Kigiriki.
  3. Kufahamu Itikadi za Jamii: Tafsiri husaidia kugundua itikadi za jamii husika. Waandishi wengi hutumia tafsiri ili kufichua imani na mitazamo yao. Hii inadhihirika kwa kuleta maoni ya jamii fulani au waandishi kuhusu masuala maalumu kupitia tafsiri.
  4. Tafsiri kama Mbinu ya Mawasiliano: Tafsiri hutumika sana katika nyanja za biashara na utalii kwa kutafsiri maelekezo ya bidhaa na huduma zinazouzwa na kusafirishwa. Pia hutumika katika vyombo vya habari na vitabu vya ufundishaji.
  5. Tafsiri kama Soko la Ajira: Wataalamu wa tafsiri wanapata ajira katika kazi mbalimbali, kama vile tafsiri za mikataba ya kimataifa, nyaraka za kisheria, na vitabu. Tafsiri pia inawawezesha waandishi kupata kipato kutokana na tafsiri za vitabu na maandiko mengine.
  6. Tafsiri Kama Mbinu ya Kujifunza Lugha: Tafsiri ni muhimu katika kukuza lugha lengwa. Kwa mfano, fasihi ya lugha lengwa inafaidika kwa kuingiza vipengele vya lugha nyingine kama vile methali na misemo, ambayo haipo katika lugha lengwa.
  7. Tafsiri katika Elimu, Sayansi na Teknolojia: Tafsiri ina mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Vitabu vilivyotafsiriwa kutoka lugha za Kiarabu kama vile Misri vilisaidia maendeleo ya nchi za Ulaya. Hali kadhalika, nchini Tanzania, tafsiri ya vitabu katika Kiswahili ilisaidia utekelezaji wa elimu ya msingi.
  8. Kueneza Fasihi Andishi na Kupanua Wasomi: Tafsiri inarahisisha upatikanaji wa kazi za fasihi kutoka katika lugha mbalimbali. Kwa mfano, Mfalme Edipode ilitafsiriwa kutoka Kigiriki hadi Kiingereza na hatimaye Kiswahili, hivyo kuleta fasihi hii kwa wasomi wengi zaidi.
  9. Tafsiri Kama Kiliwazo cha Nafsi ya Mfasiri: Tafsiri inamsaidia mfasiri kutuliza mtima wake na kuridhika na mafanikio ya kutafsiri kwa usahihi. Utafutaji wa visawe na ufanisi katika tafsiri hufanya mfasiri kufurahi na kujivunia kazi yake.
  10. Tafsiri katika Kuendeleza Dini: Tafsiri imechochea maendeleo ya dini kwa kutafsiri maandiko ya dini kutoka lugha za asili (Kiebrania kwa Biblia, Kiarabu kwa Qur'ani) hadi lugha nyingine nyingi kama Kiswahili, Kiingereza, Kijaluo, na zingine. Tafsiri hii imesababisha dini kufikia waumini wengi zaidi duniani.

Mbinu za tafsiri

  1. Tafsiri ya neno kwa neno

    Hii ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa peke yao kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha. Mdee (1986:87) anasema, "Wafasiri aghalabu tafsiri zao huhitaji neno kwa neno katika dhana fulani badala ya maelezo." Katika aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno ya lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika.

    Mfano 1: Kiswahili: Alilala hadi asubuhi. Kingereza: He/past/sleep/until/morning.

    Mfano 2: Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake. Kingereza: He/past/run/until/office/his.

    Mfano 3: Kimakuwa: mustadi anolya ishima. Kingereza: mustadi/present/eat/ugali.

    Ubora wa mbinu hii: Humsaidia mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi. Husaidia kuelewa utofauti wa mpangilio wa maumbo katika sentensi za lugha tofauti.

    Udhaifu wa mbinu hii: Upungufu mkubwa wa njia hii ni kuwa, huwa haitoi maana lengwa kwa uwazi zaidi.

  2. Tafsiri sisisi

    Hii ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa peke yao kwa kuzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:

    Kingereza: He was taken at the Central bus Station (bus). Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha mabasi. Badala ya kuwa: Alipelekwa stendi kuu ya mabasi.

    Ubora wa mbinu hii: Husaidia kufasiri dhana zisizofasirika kirahisi kama vile misemo, nahau, majina ya khanga n.k. Ni mbinu bora ukilinganisha na tafsiri ya neno kwa neno.

    Udhaifu wa mbinu hii: Si nzuri kutumika katika matini ndefu.

  3. Tafsiri ya kisemantiki

    Hii ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani limekosewa hairuhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi katika tanbihi.

    Mifano ya aina hii ya tafsiri:

    Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali. Kingereza: He went up to hospital.

    Kingereza: Aisha married Salumu. Kiswahili: Aisha alimwoa Salumu.

    Faida ya mbinu hii: Mbinu hii huingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi. Mfano lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo hiyo ni kama vile all in all - yote kwa yote, at the end of the day - mwisho wa siku.

    Udhaifu: Tafsiri hii ni ya kimzunguko na ya kiufafanuzi sana. Haina vionjo na humfikirisha sana msomaji.

  4. Tafsiri ya mawasiliano

    Ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri ana uhuru wa kutumia visawe (maneno) yanayoweza kutoa athari sawa na ilivyo katika matini chasili. Kikubwa katika aina hii ya tafsiri hulenga kuhawilisha athari iliyopo katika matini chasili hadi katika matini lengwa.

    Mfano:

    Kiingereza: Tanzania National Electric Supply. Kiswahili: Shirika la Umeme Tanzania.

    Kiingereza: Wonders never end. Kiswahili: Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.

    Kiswahili: Mwenda tezi na omo marejeo ngamani. Kiingereza: Go east, go west, home is best.

Faharasa

Baadhi ya wataalamu wameelezea mbinu tano za tafsiri wakijumlisha tafsiri neno kwa neno, sisisi, semantiki (maana), mawasiliano na tafsiri mkopo. Tafsiri mkopo ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri hutafsiri moja kwa moja mofimu za neno lililokopwa.

Mwalimu

Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.

Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.

Ingia ili kuuliza