Mada za sehemu hiiMaendeleo Ya Fasihi SimuliziMada 4
- Uwasilishaji na uenezaji wa kazi za fasihi simulizi
- Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi
- Kuhakiki kazi za fasihi simulizi
- Kutunga kazi za fasihi simulizi
Sifa kuu za kimtindo zinazotumika katika uhakiki wa hadithi / simulizi ni:
-
DHAMIRA NA MAUDHUI Ndani ya dhamira tunapaswa kulitambua wazo kuu au lengo kuu la hadithi ni jumla ya mambo yaliyomo ndani ya hadithi hiyo, yanayoibuka katika kuuendeleza wazo hilo kuu.
-
MSUKO Huu ni muundo wa hadithi yenyewe. Hapa tunaangalia jinsi matukio ya hadithi yalivyopangwa kuanzia mwanzo kwenye kitangulizi, mvuto wa hadithi ambao mgogoro kati ya wahusikawaliopo, kuwepo kwa taharuki, harakati zao hadi kwenye kilele cha hadithi au upeo, na hatimaye mwisho wake.
-
USISIMUZI Hapa tunachunguza uwezo wa hadithi wa kuweza kuiteka hadhira yake.
-
URUDIAJI Kwa kawaida urudiaji unaweza kuwa wa vipengele vya muundo, mfano: virai, maneno, sentensi, vifungu fulani, nyimbo n.k. Pia huwepo urudiaji wa mawazo, fikra, maoni n.k. Sababu za urudiaji huwa ni kufanya mambo yaliyozungumzwa kukumbukia au kusisitiza jambo fulani.
-
MATUMIZI YA NYIMBO Nyimbo hutumika kwa kiasi kikubwa katika hadithi na kufanya kazi zifuatazo:
- Kuonyesha au kusisitiza kiini au wazo kuu katika hadithi au simulizi inayohusika.
- Hushirikisha hadhira katika hadithi inayotambwa.
- Huongeza uhai wa usimulizi kwa kushirikisha hadhira.
- Huwapambanua wahusika mbalimbali wanaopatikana katika hadithi hiyo.
- Kuondoa ukinaifu unaotokana na kuutumia mtindo wa aina moja kwa kipindi kirefu.
- Kuwazindua wasikilizaji ambao huenda wakawa wamelala au kusinzia wakati hadithi inatambwa.
- Hutumika kama kiliwazo katika hadithi za kitanzi.
-
VILIWAZO / UCHESHI Ni sehemu ya hadithi ambayo huwa imekusudiwa kuituliza hadhira kidogo hasa kwenye hadithi zinazozungumzia masuala ya kusikitisha au ya kitanzia. Kiliwazo kinaweza kuwa kifungu kilichojaa ucheshi kilichokusudiwa kuondoa kwa muda ile hali ya kusikitisha. Nyimbo hutumiwa pia kama kiliwazo.
-
TAMATHALI ZA SEMI Hadithi huwa na ufundi wa kisanaa ambao hujitokeza kwa matumizi ya lugha yenye mvuto na iliyochanganya matumizi ya tamathali mbalimbali za semi. Mfano sitiari, tashibiha, tashititi, tashihisi, tafsida n.k.
-
USIMULIZI – HAKIKI / TUNDUIZI Mtambaji wa hadithi hutoa maoni kuhusu hadithi anayoisimulia. Msimulizi anaweza kutoa maoni yake kuwahusu wahusika wanopatikana hadithini au kuyahusu matukio fulani yaliyoko hadithini, kwa kiasi fulani huweza kuathiri usimulizi huu.
-
WAHUSIKA Kuna wahusika wa aina mbili katika hadithi: wahusika binadamu na wahusika ulani ambao wanapewa sifa za binadamu (mazimwi, majitu n.k.).
Katika usimulizi wa hadithi, mpaka ulipo kati ya ulimwengu wa kawaida wa binadamu na ulani hufutwa. Binadamu wanaweza kulingana, kujadiliana, kuzungumza na kuhusiana kwa jumla na ulani. Katika hadithi simulizi ulani wakubwa huweza kushindwa na ulani wadogo. Hii ni namna ya kuwakejeli wasiotumia akili zao. Viumbe wakubwa wa kudhaniwa kama mazimwi majitu husawiri kama viumbe wanaoongozwa na Tamaa kubwa, ulafi na uovu ulikithiri. Hii ni njia mojawapo ya kuziakisi sifa ambazo zinaonekana mbaya katika jamii.
Aidha kuna hadhira za aina mbili: hadhira tendi na hadhira tuli. Hadhira tendi hushiriki katika usimulizi wa hadithi mfano katika nyimbo kupiga makofi, kucheza, kuitikia, kubadilisha wasimuliaji, kuuliza, kujibu maswali na kucheza. Hadhira tuli yenyewe huwa haishiriki kwa namna yoyote ile, inapiga magoti tu.
-
TANAKALI SAUTI Mtambaji katika utambaji wake huweza kutumia sauti ambazo zinaeleza hisia au kuchora picha ya kutokea kwa jambo fulani. Pia hutumiwa kutia utamu, mvuto na msisimko wa lugha ya mtambaji, mfano: "mara cheche akatwaa zumavi akapiga, kanga pia singizia moto, ti, ti, ti……., nikamtwaa nikamfungafunga na majani ya mgomba nikampiga pu, pu, pu,…"
-
ISHARA NA TASWIRA Ishara ni matumizi ya vitu fulani kuvisimamia vingine, yaani huashiria vitu vingine tofauti. Mfano: mti mkubwa kuashiria uhusiano uliopo kati ya watu na miungu katika jamii kadhaa. Ulani ni matumizi ya lugha ambayo inamfanya msikilizaji au hadhira iweze kuunda picha akilini. Mtumiaji anaweza kutumia picha au tamathali za semi. Mfano sitiari kuunda picha hizi.
-
UTOKAJI KANDO Ni mbinu ambayo mtambaji au msimulizi anatoka kando ya utambaji wake na kutoa maoni kuhusiana na kitu kisichohusiana na hadithi moja kwa moja. Kuna utokaji kando ulani ambao unatokana na sababu zilizo nje ya hadithi yenyewe, mfano kutokana na hadhira. Utokaji kando ambao unasababishwa na nia ya kutoa maoni kuhusu tukio au kitu fulani katika hadithi yenyewe ni utokaji kando wa ndani. Hii inahusiana na usimulizi tunduzi.
-
MAIGIZO (DRAMA) SANAA ZA MAONESHO Maigizo yanatumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani. Ni sanaa inayopatikana katika makabila.
Drama za kiafrika huambatana na ngoma, utambaji, hadithi, nyimbo na matendo ya kimila (jando na unyago). Kuna maigizo yanayofungamana na michezo ya watoto, matanga, uwindaji, kilimo n.k.
-
MAIGIZO YA WATOTO Watoto wanapocheza hufanya maigizo ya matendo ya kimaisha wanayoyaona katika jamii zao mfano kulima, kufanya biashara, harusi, matanga n.k. Hizi ni sanaa za maonesho zenye kuwaburudisha na kuwaelimisha watoto licha ya kukuza vipaji vyao vya ubunifu.
-
MAIGIZO YA MSIBANI Katika baadhi ya makabila, watani au wajukuu wa marehemu hupaswa kufanya maigizo yanayohusiana na maisha, matendo au tabia za marehemu. Hii huwapunguzia wafiwa huzuni yao mbali na kutoa mafunzo fulani kwa watu waliopo msibani. Mfano tabia mbaya, maigizo hayo hupinga tabia mbaya.
-
MAIGIZO YA SHEREHE Sherehe kuu za jamii ni kama vile kuzaliwa kwa mtoto, mtoto kupewa jina, jando na unyago, harusi, kubadilisha rika, kuanua matanga, sherehe za kisiasa (mfano kutawazwa kwa mtemi), sherehe za kidini (mfano kuwakaribisha mwezi mwandamo) n.k. Kila sherehe huwa na sanaa zake za maonesho ambazo wakati mwingine huambatana na maigizo.
-
MAIGIZO YA KIDINI Maigizo hayo hufanywa wakati wa ibada, matambiko na shughuli nyingine za kidini. Katika maigizo ya aina hiyo mzimu au miungu huwa ndiyo hadhira ya igizo linalofanyika.
Uigizaji ni muhimu sana katika fasihi simulizi. Katika uigizaji huu watendaji huiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kutoa ujumbe fulani. Uigizaji huu unaweza kuwa na nia ya kukejeli, kudhihaki, kukosoa au hata kuwaburudisha. Uigizaji hautegemei sauti tu bali pia maliba mahususi kama majusoo au barakoa (maski) pamoja matendo yasiyoambatana na sauti kama michezo bubu ambayo inatilia mkazo mkubwa kwenye matendo.
Utambwaji wa hadithi unawasilishwa kwa hadhira kwa utendaji wa kisimulizi/ kitambwaji. Mashairi ni uigizaji au dhana ya aina fulani.
Mvinga ni sherehe za kiutamaduni na huweza kuhusisha matambiko. Miviga hufumbata maigizo ya aina fulani kutegemea sherehe inayohusika.
VITANZU AU VIPERA VYA MAIGIZO AU DRAMA
-
MICHEZO YA JUKWAANI Hapa pana mpangilio na mazungumzo baina ya watu na matendo yao. Mazungumzo hayo hujenga kisa ambacho kinaonesha mgogoro fulani. Kuna aina ya michezo inayoambatana na sauti na isiyoambatana na sauti kama vile ucheshi bubu, michezo bubu n.k. Onyesho bubu, kimsingi vitanzu hivi huhusisha utendaji ambao unategemea matumizi ya ishara za mikono na sehemu nyingine za mwili pasipokuwa na maneno.
-
MAJIGAMBO Haya ni maigizo ambayo yanaonesha kujitapa (yaani kujigamba) kwingi kwa mtu ambaye labda ni shujaa au ambaye ametenda mambo ya kishujaa au yenye uzito fulani. Wahusika wanaopatikana katika majigambo ndiyo watambaji au wasimuliaji wa majigambo yenyewe. Ni kawaida ya majigambo kuwa na lugha nzito iliyojaa tamathali yenye taswira au picha za undani na yenye nia na mawazo mazito.
-
VICHEKESHO Ni mpangilio wa maneno ambayo yanawasilisha ujumbe fulani maalum kwa njia ya kuchekesha au kufurahisha. Kimuundo vichekesho huwa vifupi na havihitaji uchambuzi mpevu au wa ndani ili kupata maana nyingine ya ndani. Lugha yake huweza kuwa nyepesi na iliyojaa picha ambazo watazamaji wana uwezo wa kuzitambua.
-
NGONJERA AU USHAIRI WA KIMASEMEZANO Ngonjera ni mpangilio wa tungo za kishairi za kujibizana. Ili ushairi huu uwe sehemu ya majibizano lazima uambatane na utendaji, yaani wanaohusika wanaotumia ishara za mikono, mwili, ishara za uso na nyingine ili kuwasilisha ujumbe wao. Ikiwa ngonjera haziambatani na matendo au utendaji haziwi tena sehemu ya maigizo bali sehemu ya ushairi. Mshairi mmoja anaweza kutongoa au kutunga ubeti na kutenda matendo yanayoambatana na kiini cha ubeti wako. Ngonjera, huweza kutumiwa kuwatia watazamaji au hadhira hamasa ya kutenda jambo au hata kuwasilisha maarifa fulani kwao.
-
MAZUNGUMZO Mazungumzo ni maongezi ya kimajibizano yanayotokea baina ya watu wawili au zaidi. Kigezo kikuu cha kuyafanya yawe ya kifasihi ni kuwapo kwa usanii na ufundi katika muundo wake na jinsi yanavyowasilisha ujumbe wake. Hapo juu tumeona mazungumzo ni sehemu muhimu ya michezo ya jukwaani lakini yanaweza pia kuangaliwa kivyake.
Katika jamii nyingi mazungumzo hupatikana kwa njia mbalimbali. Njia kuu za kimisingi ni kuwako kwa hotuba, malumbano kati ya watani, ulumbi au usemaji wa kiufundi wa wanajamii tofauti na pamoja na mawaidha. Hivi ni vipengele vyepesi kueleweka kwa sababu vimeenea katika jamii nyingi.
VIPERA VYA TANZU YA HADITHI KATIKA FASIHI SIMULIZI
-
NGANO Hizi ni hadithi za kimapokeo zinazotumia wahusika kama vile wanyama, majoka, binadamu, mawe, miti n.k. Fanani wa ngano hutumia maneno ya kuvuta hadhira kwa vile huanza na "PAUKWA……" ambapo hadhira hujibu "PAKAWA". Fanani huanza kusimulia hadithi yake baada ya utangulizi ambao huwavutia, huwachangamsha na kuwafanya waache kazi nyingine au kusinzia na kusikiliza ngano hiyo.
Mtambaji wa ngano wakati akiendelea kuhadithia anaweza kuuliza hadhira yake kama "niendelee? au nisiendelee?" Kauli hiyo huwafanya hadhira wasisimke na kuuitikia kwa sauti "ENDELEA!!!". Ngano hufuata muundo rahisi na wa moja kwa moja. Kwa kawaida lengo kuu la ngano ni hadithi ya kuwaasa watoto, ndiyo maana humalizia kwa kuwatia moyo kama vile wakaishi kwa raha mstarehe, wakazaa na kuzaa, maisha yakawa mazuri, amani ikatawale n.k.
-
TARIHI (VISAKALE) Hizi ni hadithi ambazo husimuliwa kutokana na matukio ya kihistoria. Matukio hayo yanaundwa kisanaa ili kuvutia watu katika jamii. Tarihi inahusu matukio yanayoweza kuwa ya furaha au huzuni na ni ya kusisimua ili kuwakumbusha watu walikotoka. Fanani wa tarihi mara nyingi pia huanza kusema "paukwa" na hadhira kuitikia "pakawa". Kuna baadhi ya masimulizi ya tarihi ambayo huanza kwa nyimbo au majigambo ambayo huwafanya wasikilizaji kuwa makini na matukio yanayosimuliwa.
Mara nyingi wahusika wa tarihi ni binadamu ambao hupewa uwezo mkubwa au mdogo mno ili kuyakinisha matukio yanayozungumziwa na kuyawekea mantiki. Tarihi anaweza kusimulia kuhusu historia ya mfalme, koo za kitawala, kumbukumbu za kutokea kwa ukoo fulani, magonjwa, vita, njaa.
-
VISASILI Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, maana na shabaha ya maisha yao. Hadithi hizi husimulia mambo yanayohusiana na maumbile ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai.
Wahusika wa visasili ambao si binadamu hupewa hadhi na uwezo wa binadamu. Kwa mfano hadithi inayohadithiwa chanzo cha chura kuwa na mabakamabaka, au jongoo kuwa na mwili ung'aao na mwororo ni kisasili. Visasili husimulia mianzo au asili ya matendo ya kufkirika, imani au mtazamo fulani katika jamii. Usimulizi wa visasili pia huambatana na nyimbo.
-
VIGANO Ni hadithi fupi zinasimuliwa kwa lengo la kuelezea makosa au uovu wa watu fulani na kutoa maadili yanayofaa. Hadithi hizi hutumia sana nahau na methali katika kutoa maadili kwa hadhira iliyokusudiwa. Maadili hayo hutolewa kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu.
Wahusika katika vigano ni wanadamu hata wanyama. Kwa kawaida vigano hujengwa juu ya tukio moja ambalo hutumiwa kuelezea juu ya maisha halisi katika jamii husika. Mara nyingi vigano havienei sana kwa jamii kwa sababu hutumiwa na muktadha wa mazungumzo.
Tamthiliya
Tamthiliya ni nini?
-
Tamthiliya (au drama) ni fani iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani.
-
Kwa lugha ya kawaida, tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza.
-
Kwa kawaida, tamthiliya huwa na masimulizi ambayo huigizwa na wahusika wa pande mbili au zaidi zinazogongana.
-
Mgongano huo husababisha mgogoro, ambapo unaposuluhishwa na kutanzuliwa, mchezo huwa umemalizika.
-
Tamthiliya ni sanaa ya maneno, hivyo ina sifa za kawaida za sanaa za maonesho ambazo ni:
- Dhana inayotendeka
- Watendaji
- Hadhira
- Kusudio la kisanaa
- Uwanja/jukwaa
- Muktadha wa kisanaa
- Ubunifu / umathilishaji
Tofauti Kati ya Tamthiliya na Sanaa Nyingine za Maonesho
-
Kwa mujibu wa Mlama:
"Tamthiliya ni aina moja wapo ya sanaa za maonyesho ambazo usanii wa utendaji wake hutegemea zaidi MATENDO na UONGEAJI, tofauti na aina nyingine kama ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji muziki."
-
Tamthiliya ni utungo ambao unaweza kuwa:
- Umeandikwa
- Haukuandikwa
-
Lengo la tamthiliya ni kuweka wazo katika umbo la tukio, ili liweze kutendeka mbele ya hadhira.
Sifa Maalum za Tamthiliya
Kitu kikubwa kinachoipambanua tamthiliya na sanaa nyingine kama vile ngoma ni:
- Msisitizo wake kwenye VITENDO na MAZUNGUMZO YA WAHUSIKA
Asili ya Neno "Tamthiliya"
-
Neno tamthiliya linatokana na neno "mithali", ambalo lina maana ya mfano au ishara ya kitu fulani.
-
Katika tamthiliya:
- Kitu kimoja humathilishwa au huwasilishwa na kitu kingine.
- Mfano: Katika mchezo wa KINJEKITILE, mwigizaji huwasilisha mhusika aitwaye KINJEKITILE.
- Mhusika huyo wa mchezo huwasilisha kwa kiasi fulani KINJEKITILE wa historia.
Aina za Tamthiliya
Zipo aina nyingi za tamthiliya kama ifuatavyo:
-
TANZIA Tamthiliya ya kijadi ya ulaya ilikuwa na matawi mawili makuu, TANZIA na KOMEDIA. Tanzia ni tamthiliya ya majonzi kuhusu anguko la mhusika mkuu. Anguko au kifo hicho huweza kusababiswa na udhaifu wake binafsi wa kitabia, kosa fulani alilofanya au mazingira fulani yaliyomzidi uwezo au mchanganyiko wa baadhi ya sababu hizo. Kwa mfano anguko la Kinjekitile na matokeo ya kosa lake binafsi (kuwafanya watu kuyaamini zaidi maji) na mazingira ya kihistoria (kisiasa na kijamii ambayo hana uwezo nayo).
-
KOMEDI / RAMSA Komedi au ramsa ni kinyume cha tanzia. Hii ni tamthiliya inayoishia katika furaha. Mhusika mkuu wa tamthiliya hupambana na matatizo ya kila aina kiasi cha kukaribia kushindwa lakini hatimaye hushinda na kufanikiwa katika malengo yake. Tamthiliya Shakespeare, Mabepari wa Venisi, shida ni ramsa.
Komedi hupendwa sana na vijana hata watu wazima kwani huwa na mvuto na ucheshi na huweza kuelimisha bila kuleta majonzi au kukatisha Tamaa. Zipo pia tamthiliya ambazo zinachanganya sifa za tanzia na komedi.
-
VICHEKESHO Vichekesho ni aina ya tamthiliya gezwa au faraguzi (zinazotungwa hapo kwa hapo bila kuandikwa). Tamthiliya hizi ziliaza miaka ya 1920 kwa lengo la kuburudisha wakazi wa mijini, wakati wa mapumziko. Tamthiliya hizo kwa kawaida zilikuwa na vituko vya kuchekesha na viliwasuta watu waliofikiriwa kuwa WASHAMBA, WAJINGA na WASIOSTAARABIKA. Hivyo mara nyingi tamthiliya hizo zilimuonyesha mhusika anayetoka shamba na kuja kuzuzuka mjini.
Vichekesho viliendelea na hata baada ya uhuru bado vipo ila dhamira zake zilibadilika. Baadhi ya vichekesho siku hizi huigizwa radioni, kwenye televisheni na kwenye vilabu vya pombe.
-
MICHEZO BUBU Hii ni aina ya tamthiliya isiyotumia maneno. Waigizaji hutumia ishara na vitendo tu, na hadhira hujua kinachotokea kwa kuzisoma ishara hizo. Tamthiliya hizi hufaa sana katika jamii zenye mchanganyiko wa watu wasiozungumza lugha moja. Zikiandaliwa vizuri na kuchanganywa na sauti za muziki au ngoma huvutia sana.
-
DRAMA NGANO Zipo drama ngano za aina mbili. Kwanza ni zile tamthiliya gezwa ambazo watoto au watu wazima huzibuni kutokana na ngano zetu za kiafrika. Ngano au hadithi simulizi huigizwa jukwaani kama drama badala ya kutambwa au kusimuliwa tu. Hii ni njia nzuri sana ya kupata michezo ya vijana shuleni. Watoto wenyewe huweza kuitunga na kuiigiza michezo hiyo kwa kuwa ngano nyingi huhusu wanyama (kwa kujipamba maleba, sauti n.k) ili kuwaigiza wahusika wanaowapenda (kwa mfano sungura). Siku hizi televisheni za ulaya zinatumia sana mbinu hii hususani katika filamu za vikatuni na vikaragosi/wanasesere (puppets).
Aina ya pili ya drama-ngano ni tamthiliya ya kimajaribio zinazojaribu kuigiza fani za jadi za kiafrika katika umbo la tamthiliya za kizungu. Katika tamthiliya hizo huweza kuwepo mtambaji ambaye huanza kwa kusema PAUKWA na mwitikiaji akajibu PAKAWA kisha mchezo huendelea kwa njia ya masimulizi na maigizo. Mifano mizuri ni tamthiliya za E. Hussein za "JOGOO KIJIJINI" na "NGAO ZA JADI" na tamthiliya za Penina Mhando za "LINA UBANI" na "NGUZO MAMA".
-
DRAMA – NGOMA Drama-ngoma ni maigizo yanayoambatana na kufungamana na uchezaji wa ngoma (dansi). Hadithi ya drama huigizwa kwa miondoko ya ngoma na nyimbo badala ya masimulizi na mazungumzo ya wahusika. Hii ni fani inayokubaliana sana na sanaa za maonesho za kiafrika na kwa vyovyote huweza kuwavutia na kuwasisimua watoto. Aidha hutoa nafasi kwa hadhira yenyewe kushiriki katika igizo badala ya kuwa watazamaji tu.
-
MICHEZO YA REDIO Michezo ya redio ni tamthiliya zinazotegemea sauti zaidi ya macho, hivyo zinahitaji mbinu maalum za kuvutia sikio ili zifanikiwe. Hadhira huwasikiliza waigizaji wanapoongea na husikia sauti au vishindo vya mambo yanayotendeka lakini huwaoni watu hao au kuyashuhudia matukio hayo. Njia hii ya maigizo huweza kuwafikia watu wengi katika eneo kubwa.
-
MICHEZO YA SINEMA, RUNINGA Hizi ni aina ya tamthiliya za kisasa zilizokusudiwa kuoneshwa katika sinema au televisheni kwa hadhira pana. Utunzi wa tamthiliya hizi unahitaji ufundi maalum, kwani uhitaji maelekezo mengi kuhusu jukwaa, mandhari, na matendo ya wahusika. Mazungumuzo ya wahusika huwa ni machache kuliko ilivyo katika mchezo wa redio au katika tamthiliya ya kawaida.
-
TAMTHILIYA GEZWA / FARAGUZI Hii ni michezo inayoandaliwa bila ya kuandikwa. Waigizaji hujitungia maneno yao papo kwa papo wakati wa onesho. Njia hii hufaa sana vijijini na shuleni hupunguza sana matatizo ya ukosefu wa tamthilia zilizoandikwa. Aidha huwa hakuna lazima ya kukariri, watoto/vijana wenyewe kujitungia michezo yao na kuigiza bila ya msaada wa mtu mzima. Hii ni njia nzuri ya kupata tamthiliya nyingi za watoto na vijana. Hata hivyo tamthiliya hizi hudai ubunifu wa uwezo mkubwa wa lugha kutoka kwa waigizaji.
Vijenzi vya Tamthiliya
Kwa mujibu wa kanuni za ki-Aristotle, tamthiliya yoyote kwa kawaida huwa na vipengele vifuatavyo:
(i) hadithi (simulio), (ii) vitendo, (iii) waigizaji wanaomathilisha wahusika wa hadhithi, (iv) daiolojia (mazungumzo). Siku hizi daolojia yaweza kuwa ya maneno au ishara.
-
HADITHI (SIMULIO) Tamthiliya husimulia hadithi au kisa fulani. Hadithi hiyo yaweza kuwa ni ya kubuni au tukio la kweli la kihistoria, au mchanganyiko wa yote mawili. Hadithi hiyo kwa kawaida inahusu mzozo fulani unaohusisha pande mbili: upande wa mbabe (shujaa wa hadithi) au nguli (mtendaji mkuu) na upande wa mpinzani wa mbabe/nguli. Hadithi hiyo husukwa kwa namna inayoujenga mgogoro wa pande hizo mbili hadi kufikia mwisho wake.
Mtiririko wa matukio kwa kawaida huwa na umbo la piramidi lenye hatua. HATUA "A" – CHANZO Katika hatua hii ndiyo huwa mwanzo au utangulizi wa mchezo. Katika hatua hii mambo yafuatayo hujitokeza:
- Usuli wa mgogoro wa tamthiliya huelezwa.
- Hali ya tamthiliya (ya majonzi, ya miujiza, ya nderemo) hudhihirishwa.
-
VITENDO KITENDO Tamthiliya hugawanyika katika sehemu kuu ziitwazo vitendo. Kila kitendo (act) huzingatia tendo kuu ndani ya mchezo, kwa mfano katika mpangilio wa matukio ulioelezwa hapo juu kila kipengele kingeweza kuwa kitendo kimoja. Hivyo tamthiliya yenye mpangilio huo kijadi ulitakiwa kuwa na vitendo vitano. Katika tamthiliya ya kijunani kumalizika kwa kitendo kuliashiriwa na kuingia kwa wazumi (chorus) jukwaani. Siku hizi zipo tamthiliya zenye kitendo kimoja, vitendo viwili, vitatu, vitano, na hata zaidi.
-
ONESHO Kila kitendo hugawanyika katika sehemu ndogo ziitwazo "maonesho". Onesho moja kwa kawaida huwasilisha tukio moja linalotendeka mahali pamoja. Kwa kawaida onesho moja hutenganishwa na jingine kwa kuzingatia mantiki ya kile kinachosimuliwa, tukio moja likimalizika onesho nalo huwa linamalizika. Wakati wa maigizo, jukwaani mabadiliko ya maonesho huashiriwa kwa kufunga pazia au kuzima taa au kwa wahusika kuondoka jukwaani.
-
WAHUSIKA NA WAIGIZAJI Usawiri wa wahusika wa tamthiliya hufanywa kwa njia ya matendo na mazungumzo, kwani fursa ya kutoa maelezo marefu haipo. Wahusika wa tamthiliya hawana tofauti kubwa na wahusika wa hadithi, huweza kuwa mviringo, bapa, watu wa tabaka la juu, wanyonge n.k. Tamthiliya huwa na wahusika wakuu na wahusika wadogo.
-
WAHUSIKA WAKUU Mbabe/Nguli: Huyu ni shujaa wa tamthiliya ambaye matendo mengi yanahusu maisha na majaliwa yake. Kwa mfano KINJEKITILE (E. Hussein 1969) ndiye mbabe au nguli (Prolagonist), yaani mhusika kiini au mtenzi mkuu.
Katika tanzia ya kijadi, mbabe aghalabu alikuwa mtu wa tabaka la juu ambaye kama tulivyokwisha elewa aliangamia kutokana na ama hila (dosari) fulani kwa tabia na maamuzi yake ama kwa sababu ya kusaka na mazingira yanayomzidi uwezo ama yote mawili, kama mfalme Odipade.
Mkinzani (antagonist): Mhusika mkuu anayepambana na mbabe au nguli.
Muwi (villain): Mhusika muovu, kwa mfano Shyloak wa Shakespeare, Mabepari wa Venisi.
-
WAHUSIKA WADOGO Hawa aghalabu huwa ni wengi na baadhi yao huwa na jukumu dogo tu katika tamthiliya. Wahusika wadogo hutokea mara kwa mara ni:
- MFOILI: Mhusika anayewekwa sambamba na nguli na aliye na sifa tofauti na za nguli kwa lengo la kuwa na kumpambanua nguli vizuri zaidi.
- MSIMULIZI: Huyu ni mhusika anayetumiwa na mtu kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu matendo na matukio katika michezo. Katika baadhi ya michezo mhusika huyu hupewa jina jingine kama mwimba.
- CHIZI (clown): Mhusika mcheshi ambaye hufanya vitu vya kipumbavu na kusema maneno ya kijingajinga ili kuiburudisha hadhira na wakati mwingine kutoa ujumbe fulani.
- WAIGIZAJI: Waigizaji pengine huitwa wamathilisha, ni watu wanaotokea jukwaani mahala pa wahusika wa mchezo na kwa vitendo na tabia za hao wahusika wamathilisha. Waigizaji hawana budi kuteuliwa vizuri ili wawakilishe na kuwasilisha sawa sawa umbo, hali, hisia, tabia, mawazo, na matendo ya wanaomathilisha.
-
DAIOLOJIA (MAZUNGUMZO YA WAHUSIKA) Hadithi ya tamthiliya husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Mazungumzo ya wahusika ndio huitwa daiolojia. Mafanikio ya michezo mingi hutegemea namna mtunzi anavofaulu kuweka daiolojia inayovutia na kuaminika.
Daiolojia ni lazima iwe na maneno machache yaliyoteuliwa vizuri ili kuisogeza mbele hadithi au kudhihirisha jambo fulani alilokusudia mtunzi.
Baadhi ya tamthiliya huwa na monolojia pia. Katika monolojia mhusika huzungumza mwenyewe kudhihirisha mawazo aliyonayo moyoni. Zipo pia tamthiliya zinazotumia masimulizi ambapo hutokea masimulizi na kusimulia au kusimulia mambo yaliyotokea, mithili ya mtambaji wa hadhithi au utendi. Mbinu hii hutumika katika drama tendi. Baadhi ya tamthiliya za Kiswahili kwa mfano M. Mulokozi katika MKWAWA WA UHEHE zimetumia mbinu hizi.
Mbinu Nyinginezo katika Tamthiliya
-
Watunzi wa tamthiliya za Kiswahili wametumia mbinu mbalimbali, baadhi zikiwa zimeigwa kutoka katika fasihi ya Kimagharibi.
-
Tamthiliya nyingi zina:
- Muundo wa Ki-Aristotle
- Daiolojia (mazungumzo baina ya wahusika)
- Vitendo, maonyesho, na migogoro inayosuluhishwa mwishoni
-
Baadhi ya tamthiliya zimeiga mbinu za sanaa za maonesho za jadi za Kiafrika:
Mifano ya Watunzi na Mbinu Walizotumia
-
Ebrahim Hussein:
- Alitumia mbinu za utambaji wa katika:
- Ngano za Jadi
- Jogoo Kijijini
- Hadi sasa wataalamu hawajakubaliana kama tungo hizi ziitwe tamthiliya au tendi.
- Alitumia mbinu za utambaji wa katika:
-
Penina Mhando:
- Katika Lina Ubani na Nguzo Mama, alitumia mbinu ya utambaji wa ngano.
- Alitumia mbinu ya majigambo katika Harakati za Ukombozi (pamoja na wenzake).
-
Mbogo:
- Alitumia mbinu ya majigambo katika Sundiata.
-
Mlokozi:
- Alitumia mbinu ya tendi simulizi katika Mkwawa wa Uhehe.
Hitimisho
- Mbinu hizi hutumiwa na watunzi ili kuzifanya tamthiliya zikaribiane na utamaduni wa jamii husika.
- Zinasaidia kufanya kazi ya tamthiliya kuwa ya kitaifa, kijadi na halisi kwa mazingira ya Kiafrika.
Mwalimu
Unasoma somo hili? Niulize nikuelezee chochote kilichomo.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu mada hii.
Ingia ili kuuliza