Mada za sehemu hiiHotubaMada 1
- Hotuba
Hotuba ni mazungumzo yanayofanywa na mtu kuhusu suala fulani mbele ya kikundi cha watu. Hotuba inaweza kutolewa na mwananasiasa kwa wananchi, walimu kwa wanafunzi, au mhubiri kwa waumini.
Hotuba hujikita kwenye suala kuu fulani, na inaweza kutolewa bila kuandaliwa. Hata hivyo mara nyingi hotuba huandikwa ili kumtayarisha msemaji vilivyo kuhusu lugha atakayoitumia, masuala atakayoyaongelea na mtiririko wa mawazo. Hata hivyo, hotuba nzima huwa haiandikwi, kwani kuna haja ya atakayeitoa kutayarisha vidokezo vya kumwelekeza.
- Kuelimisha watu, mfano jinsi ya kujikinga na Korona (Covid-19).
- Kutoa habari, mfano Waziri wa Elimu kueleza mabadiliko ya mtaala wa elimu.
- Hotuba hupata jina lake kutegemeana na mada yake. Inaweza kuwa hotuba za kiafya, kisiasa, kielimu, kimazingira n.k.
Kichwa cha Hotuba
Kichwa, anwani, hurejelea mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.
Mfano: Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya madawa ya kulevya kwa wananchi.
Utangulizi
Kipengele hiki ni kwa ajili ya kuwatambua waliohudhuria katika mkutano. Ni vema kuwataja majina kwa kuanzia na yule wa cheo cha juu hadi wa cheo cha chini.
Pia ni vema kujitambulisha kwa hadhira hasa ikiwa unazungumza na hadhira isiyokujua au wageni.
Mfano:
Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha mazingira, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu heri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa kikundi cha mazingira na mchana wa leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili tuboreshe mazingira yetu.
Kiini
Sehemu hii ni muhimu kwani ndiyo sehemu yenye hoja na mawazo. Hakikisha kila hoja imeandikwa kwenye aya yake yenye sentensi kuu. Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho na ujumbe unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
Tamati
Tamati inaweza kuwa na mitindo mingi. Unaweza kumalizia kwa usemi, ama unaweza kumalizia kwa kusisitiza hoja muhimu katika hotuba. Ni katika sehemu hii hadhira huweza kupewa changamoto kuhusu suala kuu la hotuba. Mfano, kama hotuba ni ya kutunza mazingira unaweza kuuliza hadhira, Je, tukizidi kuharibu vyanzo vya maji tutapata wapi maji ya kutumia pindi vyanzo vitakapokauka? Pia, kumbuka kuwashukuru watu kwa kuhudhuria. Msimamo wa hotuba usisitizwe hapo.
Uandishi wa hotuba unatakiwa kuzingatia mambo kadhaa. Mambo hayo ni:
- Kuchagua jambo la kuzungumza
- Kujua kusudio la kutoa hotuba kama ni kushawishi, kuelimisha au kuonya
- Kubaini aina ya hadhira unayohutubia, mfano, watoto, wazee, wanakijiji, wanafunzi, wasomi, au waumini wa dini
- Kujielimisha kuhusu mada inayohusika. Hii inaweza kuwa ni kwa njia ya kusoma vitabu au kuwauliza wataalamu
- Kutumia lugha inayoendana na mada pamoja na hadhira inayohusika
Utoaji wa hotuba ni jambo tofauti sana na utayarishaji. Kuna watu walio na uwezo wa kutayarisha hotuba nzuri lakini hawawezi kuitoa kikamilifu kwa hadhira.
Mambo yawezayo kumwongoza mtoaji hotuba:
- Ni muhimu kuzingatia muda wa hotuba ili usiwachoshe wasikilizaji wako. Hotuba isiwe fupi wala isiwe ndefu kupindukia ikiwaudhi wanaosikiliza.
- Hakikisha umezingatia hadhira katika utayarishaji vilevile, katika utoaji hakikisha hadhira imezingatiwa. Chagua lugha inayofaa kwa hadhira yako.
- Hakikisha unafanya mazoezi ya sauti, lugha na kusimama mbele ya hadhira kabla ya kutoa hotuba.
- Hakikisha umevaa vizuri na kuonekana nadhifu mbele ya watu.
- Kumbuka unazungumza na hadhira hai hivyo maneno ya hotuba yako lazima yashawishi.
- Zingatia kasi inayofaa; usizungumze haraka haraka mno wala polepole sana.
Hotuba ya Diwani wa Kata kwa wananchi wa kijiji cha Kirisha kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji.
Kirisha hoyee!
Ndugu mwenyekiti wa kijiji, ndugu katibu wa kijiji, ndugu wanakijiji wote mabibi na mabwana. Ninayo furaha kusimama mbele yenu na kuzungumza. Nikiwa kama mwanaharakati wa muda mrefu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, leo ninasimama tena mbele yenu kuwaeleza na kuuthibitishia umma huu kuwa maji ni uhai.
Asilimia sabini ya miili yetu ni maji. Hivyo bila maji mwanadamu hawezi kuishi. Sisi ni maji, hivyo lazima tuishi kwa tahadhari kubwa kuyanusuru maji haya yasipotee tukaadhirika.
Laiti kama tungepata nafasi ya kutembelea watu waishio jangwani, tukawaona jinsi wanavyopata shida ya maji tungejifunza kitu. Vipo visa kadhaa vimekuwa vikiripotiwa katika vyombo vya habari kuhusu watu na wanyama waliokufa kwa ukosefu wa maji.
Ukiachilia mbali matumizi yetu, hata viumbe wengine kama mamba, samaki, viboko, nao wanategemea maji haya ili waendelee kuishi. Ndugu zangu lazima sasa tukubaliane kuwa maji ni uhai.
Ni kipi hakihitaji maji? Hata viwanda vyetu hivi tunavyovitegemea kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali vinahitaji maji ya kupoozea mitambo.
Wanyama na mimea ni vitu ambavyo tunavitegemea kwa chakula pia vinahitaji maji. Kilimo bila maji ni sawa na sifuri. Bila maji wote tutakwisha na kusahaulika mara moja.
Niwaombe ndugu zangu, tuache mara moja hii tabia iliyozuka hivi karibuni. Tabia ya kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji pamoja na kukata miti hovyo. Hii itatuletea balaa. Hatukatazi kukata miti, lakini hakikisha unapokata mti uwe na kibali maalumu, kwani unatakiwa kupanda mti ndipo ukate mti.
Ni matumaini yangu makubwa mtayafanyia kazi vile nilivyoyasema. Kimsingi zaidi, tuhakikishe tunaepuka tabia zote ambazo zitatuharibia vyanzo vyetu vya maji.
Mwisho niwashukuru wote mliohudhuria na kunisikiliza, nasema asanteni sana.
Kufupisha habari au hadithi aliyoisoma kwa kutumia maneno yake na kubainisha mawazo vyote ya msingi ya mwandishi na kuyaelezea kwa usahihi.
Habari ni mawasiliano ya maarifa kuhusu matukio ambayo huwasilishwa kwa mtu au watu kwa maneno ya kinywa, kwa maandishi kama vile magazeti, kwa matangazo ya masafa marefu kama vile redio au runinga, na kwa intaneti.
Ufupisho wa habari ni kuelezea upya jambo kwa maneno machache zaidi bila kupoteza maana ya msingi. Kwa kawaida idadi ya maneno inatakiwa kuwa theluthi ya habari ya awali. Uwezo wa kufupisha unatumika kama kigezo kimojawapo cha kupima uelewa wa mwanafunzi.
Swali
Sehemu gani ya hotuba hurejelea mada na hadhira?
Ingia ili kuwasilisha jibu lako na lihesabiwe katika umahiri wako.
Ingia ili kufanya mazoeziMwalimu
Umekwama? Niulize chochote kuhusu mada hii.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu swali hili.
Ingia ili kuuliza