Mada za sehemu hiiAina Za ManenoMada 1
- Aina za Maneno
NENO
Neno ni sehemu fupi ya lugha yenye maana. Ni sauti inayotamkwa au kuandikwa pamoja na kutajajambo fulani. Neno linaweza kuwa fupi lenye mofimu (yaani sauti inayowakilisha maana fulani) moja tu au kuwe refu lenye mofimu mbalimbali. Kwa kawaida ni muunganiko wa silabi kadhaa. Mfano ba + ba = baba. Irabu u + a = ua.
Aina za maneno uhusisha mgawanyo wa maneno hayo kulingana na matumizi yake. Zipo ama saba za maneno ambazo ni:
Nomino hufanya kazi ya kutaja jina la mtu, kitu hali au mahali. Mfano: baba, Tanzania, ugonjwa n.k. Baba analima, chakula kimemwagika
Zipo aina mbalimbali za nomino ambazo ni:
- Nomino za kawaida
Nomino hizi hazibainishi waziwazi vitu vinavyotajwa. Ikiwa ni mtu hatambuliwi kama ni Juma au Asha, ikiwa ni mlima hautambuliwi kama ni Kilimanjaro, Meru, hutaja kwajumla. Mfano: baba, mvulana, mji, nchi. Nomino hizi kwa jina jingine huitwa nomino za jumla.
Mfano:
- Rafiki yangu amekufa
- Baba analima
- Nomino za kipekee
Nomino hizi hutaja na kutambulisha nomino mahsusi na kipekee. Yaani kitu ni hicho hicho wala si kitu kingine. Mfano: Juma, Arusha, Mlima Kilimanjaro n.k. Herufi za kwanza za nomino za kipekee huwa ni kubwa hata kama nomino hizo zinapatikana katikati ya sentensi.
Mfano:
Maryam anafua nguo.
- Nomino za jamii
Hizi ni nomino zinazowakilisha vitu vingine katika jina moja. Yaani hutaja ujumla wa vitu vingi. Mfano: Jeshi, timu, mkutano, kamati.
Timu yetu ilishinda kwa kishindo.
- Nomino dhahania
Hizi ni nomino zinazofikiriwa pasipo kuonekana.
Mfano: Malaika, Zimwi, Jini.
- Nomino za wingi
Nomino hizi hudokeza dhana ya wingijapokuwa zenyewe hazina wingi wala umoja. Umbo la nomino hizi linafanana na nomino zilizo katika wingi japokuwa mfano huo ni wa bahati tu.
Mfano: maziwa, maji, manukato, majadiliano.
Maziwa vamemwagika.
- Nomino za matendo
Nomino hizi huonesha matendo.
Mfano: ukulima, ufugaji, mapigano.
Mapigano yalizuka mjini.
Haya ni maneno yanayotoa taarifa ya ziada katika nomino. Hufanya kazi ya kufafanua kuelezea zaidi kuhusu nomino ili kupambanua kutofautisha nomino husika miongoni mwa nomino nyingine.
Mfano:
Mtoto wangu amefaulu, yule mpole amesafiri.
- Vivumishi vya idadi
Vivumishi hivi hutumika kueleza kuhusu idadi ya nomino. Yaweza kuwa idadi isiyodhihirika. Mfano: wengi, wastani, nyingi n.k au idadi halisi. Hapa nambari hutumika kueleza idadi ya nomino, mfano: kumi, elfu.
Mfano:
Watu wengi waliabudu sanamu lakini watatu walikataa.
- Vivumishi wa sifa
Hivi hutumika kutoa sifa za nomino mbalimbali, mfano: kali, safi, mfupi, mnene n.k
Mfano:
Yule kijana mrefu ana pua kubwa
- Vivumishi viulizi
Hutumika kuuliza swali, mfano: gani? yupi?
Mtoto yupi amevunjika?
- Vivumishi wa a - unganifu
Vivumishi hivi huundwa kwa mzizi wa kihusishi a - unganifu. Kihisishi hiki huandamana na nomino kuunda kirai husishi ambacho huvumisha nomino iliyotajwa awali.
Vivumishi hivi huleta dhana za umilikaji wa nomino na nafasi katika orodha.
Mfano: ya, cha, za.
Nguo zajuma zilianguka alipocheza.
- Vivumishi wa kumiliki
Vivumishi hivi hutoa taarifa ya kujulisha umiliki wa nomino. Maneno yake hujulisha kuwa nomino hiyo iliyotajwa ni mali ya nani.
Mfano: yangu, wao, wenu.
Nyumba yangu imebomoka
- Vivumishi wa kuonesha
Vivumishi hivi hutoa taarifa ihusuyo nomino au kiwakilishi cha nomino kwa kudokeza umbali au ukaribu wa nomino iliyotajwa. Umbali huo unaweza kuwa karibu: mbali kidogo au mball sana. Pia tunaweza kuvitupia katika wingi au umoj a tukizingatia ngeli za nomino na upatanisho wa kisamfi.
Mfano: kile, ile, hii.
Kidumu kile ni changu.
Jembe hili limevunjika.
Haya ni maneno yanayosimama badala ya nomino. Maneno hayo hutumika pale tu ambapo nomino haipo au haikutajwa, huenda kwa kuwa imeshatajwa hapo awali au inafahamika katika mazingira husika.
Mfano:
Mimi ni mwalimu.
Wote wamepotea.
Zipo aina mbalimbali za viwakilishi ambazo ni:
- Viwakilishi wa kuuliza viulizo
Viwakilishi hivi husimama badala ya nomino iliyoulizwa.
Mfano:
Nani anagonga?
Lipi ni zima?
Mangapi ni mabovu?
- Viwakilishi wa sifa
Viwakilishi hivi huonesha sifa za nomino zinazowakilisha.
Mfano:
Mfupi amelala
Mjinga kaondoka
Mchangamfu anakuja kesho
- Viwakilishi wa idadi
Viwakilishi hivi hujulisha idadi ya watu au vitu. Idadi inaweza kuwa yajumla au kamili.
Mfano:
Wanne wamekamatwa (idadi kamili)
Wengi hawakufika (idadi ya jumla)
- Viwakilishi wa kuonesha mahali
Haya ni maneno yanayosimama badala ya nomino ili kujulisha kudokeza ukaribu au umbali wa nomino hiyo ambayo hutoka kwa mzungumzaji.
Mfano:
Yule ni mvivu
Wale wameondoka
Hili limeiva
- Viwakihshi wa nafsi
Haya ni maneno yanayosimama badala ya majina yanayotaja nafsi za watu. Viwakilishi vya nafsi vimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
-
Viwakilishi vya nafsi huru
-
Viwakilishi vya nafsi kiambata
-
Viwakilishi vya nafsi huru
Haya ni maneno yanayoweza kusimama peke yake bila kuambatanishwa katika neno au mzizi wa neno jingine.
Mfano:
- Mimi ni mkulima
- Ninyi ni wakulima
- Sisi ni walimu
- Yeye ni mwalimu
- Wao ni walimu
- Viwakilishi vya nafsi kiambata
Hizi ni mofimu tegemezi. Vipande vya maneno vinavyoambikwa au vinavyoambatanishwa katika neno au mzizi wa neno jingine ili kudokeza nafsi inayohusika.
Mfano:
- Viwakilishi wa kumiliki vimilikishi
Hivi huonesha umiliki na umiliki huo huhusishwa moja kwa moja na nomino inayohusika.
Mfano:
Kwetu ni karibu
Kwao ni walevi
- Viwakilishi wa-a- unganifu
Haya ni maneno ya sifa yanayosimama badala ya nomino inayosifiwa kwa kutumia -a- unganifu.
Mfano:
La saba wamemaliza
Vya China ni feki
- Viwakilishi wa urejeshi virejeshi
Haya ni maneno yanayorejelea nomino ambayo haikutajwa. Maneno hayo huwa na kirejeshi kinachorejelea na nomino yenyewe haitajwi.
Mfano:
Aliyemaliza aondoke
Lililoiva litaliwa leo
Alimoingia mna vumbi sana
- Viwakilishi wa pekee
Hivi hubainisha nomino ambayo hutajwa kwa kutumia viambishi vya:
-ote, -o-ote, -enye-, -enyewe-, na -ingine.
Viwakilishi hivi huitwa vya pekee kwa sababu kila mmoja hutoa taarifa fotauti (ya peke yake) na chenzake. Kimsingi mizizi yake ipo mitano.
MCHANGANUO:
- -ote
Maana hasa ya hali ya "kutokubaki na kitu" ukiwa mazungumzoni
Mfano:
Yote yamemwagika
Zote zimeharibika
Chote kimeliwa
- -o-ote
Maana hasa ni hali ya kutokuchagua "pasipo uchaguzi"
Mfano:
Yeyote aje
Lolote liwe
Zozote zitapendezwa
- -enye-
Maana hasa ni hali ya "umiliki"
Mfano:
Mwenye nyumba amefariki
Vyenye sukari vimeharibika
- -enyewe-
Maana hasa ni hali ya "msisitizo"
Mfano:
Yenyewe imepasuka
Chenyewe kimetoboka
Kwenyewe kumenuka
- -ingine
Maana hasa ni hali ya "nyongeza"
Mfano:
Mwingine amefariki
Kingine kimepotea
Nyingine imepauliwa
Vingine vimeletwa
- Viwakilishi wa amba
Haya ni maneno yanayosimama badala ya nomino kwa kutumia mzizi wa amba.
Mfano:
Ambaye amemaliza aje
Ambazo zimeoza zitatupwa
Ambacho kina sumu kimechomwa
Haya ni maneno yanayotoa taarifa ihusuyo kitenzi. Maneno hayo huelezea hufafanua na kupambanua au kuongeza maana zaidi ya namna jinsi tendo linavyotendeka, Idadi au kiasi cha kutendeka kwa tendo hilo, mahali ambapo tendo linatendeka. Hivyo vielezi ni maneno yanayotoa taarifa ili kukijulisha kitenzi hicho kimetendeka kwa namna gani, au jinsi gani: mara ngapi au kwa kiasi gani, wapi, lini na kwa sababu gani. Wakati mwingine vielezi hutoa taarifa inayohusu nomino, viwakilishi, vivumishi na hata vielezi vyenzake.
Zipo aina mbalimbali za vielezi nazo ni:
Vielezi wa namna
Haya ni maneno yanayotoa taarifa au ufafanuzi ambao unaelezea namna aujinsi kitenzi (tendo) linavyofanyika na maneno haya hujulisha kuwa kitenzi hicho kinatumika namna gani aujinsi gani.
Vielezi hivi vya namna vimegawanyika katika makundi madogomadogo sita, ambayo ni:
Vielezi halisi
Vielezi hivi kazi yake ni kutoa taarifa ihusuyo kitenzi
Mfano:
Nyoka anakimbia sana
Hadija anaandika vizuri
Asha amejikwatua mno
Vielezi vinavyofafanua vivumishi
Mfano:
Baba amenunua njumba nzuri sana
Ndondi si mchezo nzuri kabisa
Vielezi vya ki-ya mfanano
Mfano:
Halima anaimba kitoto
Rahimu amevaa kiuni
Vielezi vya hali
Vielezi hivi vina uhusiano na tabia ya kitu. Nomino za dhahama zinapotumika kufafanua kitenzi huwa kielezi.
Mfano:
Barabara zetu zimejengwa upya
Gari hili hukimbia kwa kasi
Vielezi viigizi
Hivi hufuatisha huiga mlio unaotokea baada ya tendo kutendeka.
Mfano:
Maji yamemwagika mwaa
Ali ameanguka puu
Vielezi vikariri/vibariki/viradidi
Haya ni maneno yanayofafanua kielezi kuwa kitenzi hicho kimetendeka mara ngapi au kwa kiasi gani. Idadi hiyo inaweza kuwa idadi yajumla au idadi kamili.
Mfano:
Mtoto anatembea polepole
Ali analima kinyumenyume
Vielezi vya idadi
Haya ni maneno yanayofafanua kielezi kuwa kitenzi hicho kimetendeka mara ngapi au kwa kiasi gani. Idadi hiyo inaweza kuwa idadi yajumla au idadi kamili.
Mfano:
Jamali ameanguka mara nyingi
Makande hupikwa mara mbili
Gari lilipinduka mara tatu.
Vielezi vya mahali
Ni maneno yanayofafanua kwa kujulisha mahali ambapo kitenzi hicho kinatendeka kimetendeka.
Mfano:
Mtoto amelala chumbani
Mama amekwenda shambani
Panya amejificha shimoni
Vielezi vya mahali hujengwa kwa kuambikwa kuambatanishwa na "ni" mwishoni mwa nomino inayokubali upatanisho wa kisarufi baada ya kuongezewa hiyo ni mwishoni mwake.
Vielezi wa wakati
Ni maneno yanayofafanua kielezi kwa kujulisha wakati ambao kitenzi hicho kinatendeka kimetendeka.
Vielezi vya wakati vinaweza kuwa vya majina ya siku, wiki, mwezi, majira ya mwaka, nyakati za siku, matukio ya kihistoria n.k
Mfano:
Wakulima hupanda wakati wa masika
Jambaz1 sugu limeuawa jana usiku
Nitasafiri wiki ijayo
Mimi nilizaliwa wakati wa vita vya majimaji
Vielezi viulizi
Hivi huulizajuu ya tendo linavyofanyika, lilipofanvika, lililotendwa, lilipofanywa.
Mfano:
Baba amenunua nini?
Asha anasoma wapi?
Haya ni maneno yanayoelezajambo lililotendwa. Vitenzi huarifu tendo lililofanyika au litakalofanywa na mnyama, mtu au kiumbe cho»chote kinachoweza kutenda jambo.
Mfano: cheza, lima, panda, imba.
Mara nyingi vitenzi huwa havisimami peke yake vinatumika katika tungo, bali huambatana na viambishi vingine vyenye kuwakilisha mtenda au mtendwa wajambo. Vilevile huambatana na viambishi vyenye kuonesha wakati wa tendo lilipofanvika.
Mfano:
Baba analima (a— na- lima)
Watoto wanacheza (wa — na- cheza)
Wazungumzaji wa Kiswahili hutumia vitenzi pamoja na viambishi ili kuonesha nafsi ya mtenda na pia wakati tendo lilipofanvika. Ni mara chache sana ambapo wazungumzaji hutumia vitenzi visivyochukua viambishi. Hali hii hutokea wakati mzungumzaji anapotoa amri. Mfano: imba, tembea, simama.
- Kitenzi kikuu (T)
Ni kitenzi ambacho hutoa wazo kwa tendo ambalo linatendwa na nomino au kiwakilishi cha nomino. Mara nyingi kitenzi kikuu hukaa peke yake katika sentensi na hutoa taarifa kamili bila ya kuhitaji msaada kitenzi kingine.
Mfano:
- Baba yangu anacheza vizuri
- Shamba langu limepandwa mahindi
- iii. Sisi tunasoma Kiswahili
SIFA ZA KITENZI KIKUU (T)
- Huweza kusimama peke yake katika tungo au sentensi na kukamilisha taarifa bila ya kuwepo kitenzi kingine.
Mfano:
Mania anakula
- Huweza kuonesha ukanushi au uyakinishi
Mfano:
Ali anakimbia (uyakinishi)
Wewe hutacheza kwaito (ukanushi)
- Kitenzi kisaidizi (Ts)
Kitenzi hiki hukaa sambamba na kitenzi kikuu ili kusaidia kukamilisha taarifa. Kitenzi kisaidizi kikiwa peke yake hakiwezi kutoa taarifa kamili: hivyo basi kinahitaji kitenzi kingine ndipo taarifa yake ikamilike.
Mfano:
Mtoto aliyekuja ameondoka
Bibi yangu alikuwa anaumwa
- Kitenzi kishirikishi (t)
Hiki ni kitenzi ambacho hujulisha hali ya kuwepo au kutokuwepo kwa uhusiano na ushirikiano baina ya vipashio vya lugha. Uhusiano huo unaweza kuwa katika tabia, haili au mazingira fulani.
Mfano:
Juma ni mwizi
Kikombe kichabati
- Vitenzi vishirikishi vikamilifu:
Haya ni maneno ambayo vamekamilika yaani hayahitaji mofimukiambishi silabi neno au kitenzi kingine.
MIZIZI YA VITENZI VISHIRIKISHI:
- Kuwa:
Endapo utakuwa na kitenzi cha mzizi wa kuwa kimekaa peke yake katika sentensi na kimetoa taarifa kamili basi hicho ni kitenzi kishirikishi.
Mfano:
Ali alikuwa mtulivu darasani
Fatuma hakuwa mtoro
- Ni:
Hiki ni kitenzi kishirikishi kinachojulisha uyakinishi wa tendo. Kitenzi hiki hujulisha kuwepo kwa uhusiano baina ya vipashio vya lugha.
Mfano:
Juma ni mcheshi
Simba ni mnyama mkali
- Si
Hiki ni kitenzi kishirikishi kinachojulisha ukanushi wa tendo. Kitenzi hiki hujulisha kuwepo kwa uhusiano baina ya vipashio vya lugha.
Mfano:
Halima si mchokozi
Asha si mtiifu
Abi si mwimbaji
- Vitenzi vishirikishi vinavyojulisha umiliki
Hivi ni vitenzi vinavyotoa taarifa ya umiliki kwa nomino au kiwakilishi.
Mfano:
Juma ana gari zuri
Chakula kina mafuta mengi
Juma ana mke mzuri
Chatu hana nnguu
- Vitenzi vishirikishi vya viambishi ngeli
Hivi ni vitenzi vinavyoainisha maana ya ngeli nusimama peke yake.
Mfano:
Ndoo iko bwawani
Kikombe kiko kabatini
Jembe liko shambani
- Vitenzi vishirikishi vipungufu:
Hivi ni vitenzi vyenye mzizi wa "ndi". Vitenzi hivi hujulisha msisitizo wajambo. Vitenzi vishirikishi vipungufu huchukua viambishi vya nafsi na viambishi vya ngeli ya urejeshi.
Kuna mizizi miwili ya vitenzi vishirikishi vipungufu navyo ni nafsi na ngeli za urejeshi.
- Nafsi
Mfano:
Mimi ndimi mjukuu wao
Wewe ndiwe mwalimu wao
Ninyi ndinyi walimu wao
Wao ndio walimu
- Vya ngeli ya urejeshi
Mfano:
Humu ndimo alimoingia
Hiki ndicho kitabu chake
Hizi ndizo ndizi zake
Bainisha vitenzi katika sentensi zifuatazo:
- Baba na mama wanalima. (T)
- Mtoto aliyeondoka amegongwa na gari. (Ts)
- Ali si mvivu (t)
- Chakula kina chumvi nyingi. (t)
- Darasa la saba wanasoma kwa bidii. (T)
- Mwalimu alijeruhiwa amefariki. (Ts)
- Jembe li shambani. (t)
Viunganishi ni neno au kikundi cha maneno chenye kuunganisha vipashio vya lugha ili kuunda kipashio kikubwa zaidi. Pia ni maneno yanayounganisha maneno mengine. Kiunganishi kinaweza kuunganisha neno na neno, kirai na kirai, kishazi na kishazi, sentensi na sentensi au vinginevyo.
Mfano:
- Baba na mama
- Mama anafua na baba anasoma gazeti
- Shoka limeshindwa sembuse kwanja
Maumbo ya viunganishi ni:
Na, lakini, ingawa, bila, sembuse, ila, kwa sababu, kwa kuwa, pamoja na, iwapo, labda n.k
Zipo aina mbili za viunganishi navyo ni:
- Viunganishi huru
Hivi ni viunganishi vinavyosimama peke yake katika tungo katikati ya vipashio vinavyoungwa.
Mfano:
Sisi tunaimba na kucheza
Baba anafua lakini mama amelala
- Viunganishi tegemezi
Hivi ni vile ambavyo huundwa kwa viambishi vya urejeshi vinavyowekwa katika kishazi huru kwa pamoja kuunda sentensi changamano. Viambishi hivyo ni kama vile: po, ye, lo, cho.
Mfano:
Mama anayepika ni mchaga
Aliowaona aliwataja.
Bainisha viunganishi katika sentensi hizi:
- Karanga na mtama hupandwa shambani. (U)
- Anasoma ingawa anaumwa. (U)
- Ashura aliondoka kisha Juma akamfuata. (U)
- Hakuja shule kwa kuwa alikuwa anaumwa. (U)
- Mimi nimeshindwa kukwea mti sembuse wewe. (U)
Vihisishi ni maneno yanayodokeza vionjo na miguso ya moyo au ya akili.
Vionjo vya moyo huweza kuwa vya furaha au huzuni. Maneno hayo kwa kawaida huwepa alama ya mshangao (!) au hutengwa kwa mkato (,) yatokeapo katika maandishi. Mfano wa maneno hayo ni Loo! Ebo! La hasha! n.k
Kila kihisishi huweza kuibua hisia mahsusi: kwa hiyo ni vyema kutumia kihisishi kinachofaa.
Mfano:
Lo! Maajabu ya Musa hayo!
Salale! Angalia alivyochafuka!
Swali
Neno ni nini?
Ingia ili kuwasilisha jibu lako na lihesabiwe katika umahiri wako.
Ingia ili kufanya mazoeziMwalimu
Umekwama? Niulize chochote kuhusu mada hii.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu swali hili.
Ingia ili kuuliza