Sonzaschool
Rudi

Msingi · Darasa la Saba

Kiswahili

Mashairi ya Kisasa

takriban dakika 4 kusoma

Mada za sehemu hiiMashairiMada 2
  1. Mashairi Ya Kimapokeo
  2. Mashairi ya Kisasa

MASHAIRI YA KISASA

Mashairi ya kisasa ni mashairi yasiyozingatia kanuni za muwala, urari wa mizani, vina, na idadi maalum ya mistari katika kila ubeti. Mashairi haya pia hujulikana kama mashairi ghuni, masivina, au mapingiti.

Tofauti na mashairi ya kimapokeo, mashairi ya kisasa hayatumii vina na mizani kujenga mdundo, badala yake, hutegemea matumizi ya viwango mbalimbali vya lugha kama vile mofolojia, sarufi, na mantiki. Viwango hivi huweza kutumika kuleta muwala au mtiririko mzuri wa habari.

Sifa za Mashairi ya Kisasa

  • Hutegemea sifa za kisimu na kimantiki.
  • Hutumia mnyambuliko wa maneno kwa mtiririko wa maana.
  • Hutumia mpangilio wa mshororo unaotegemea dhamira.
  • Ruwaza za mishororo na beti hubadilika kulingana na mtunzi.
  • Mishororo inaweza kuwa mifupi au mirefu bila kufuata mpangilio maalum.
  • Hutumia takriri nyingi ili kusisitiza ujumbe.

Mfano wa Shairi la Kisasa

Busara na maarifa ni sawa na ujinga na upumbavu, Furaha na kicheko ni sawa na kilio na huzuni, Njia yenye mwanga ni sawa na njia yenye giza, Ukitenda wema unaweza kulipwa mabaya. Mwenzako akimwaga ugali, Wewe mwaga unga: Na mwenzako akimwaga mboga, Mwaga mafuta. Lakini yote haya yataisha, Binadamu wenzangu, Tambueni dunia imegeuka, Mbele kumekuwa nyuma, Na nyuma kumekuwa mbele, Dunia imegeuka kuwa tambara bovu, Ukilishika linachanika, Dunia sasa mti mkavu, Usiofaa kuchimba dawa.

Tofauti kati ya Mashairi ya Kimapokeo na Mashairi ya Kisasa

SifaMashairi ya KimapokeoMashairi ya Kisasa
Vina na MizaniHuzingatia vina na mizaniHayazingatii vina na mizani
Mpangilio wa BetiHuwa na idadi maalum ya mistari katika kila ubetiHauna idadi maalum ya mistari
Mtindo wa LughaHutumia lugha yenye mpangilio wa kimuzikiHutumia lugha yenye uhuru wa ubunifu
TakririHaitumii takriri mara nyingiHutumia takriri kusisitiza ujumbe

SHAIRI LA KIMAPOKEO

Nisaidieni jamii, enyi majirani zangu, Nanyi wapita njiani, mwiione hali yangu, Kumezuka manyumbani, meniruka ndugu zangu, Nala nanywa mapipani, hali yangu taabani. Sina baba wala mama, sina babu sina nyanya, Sigambi mie yatima, wandugu watanisonya, Nanyimwa hata kulima, jamani nini tafanya, Nala nanywa mapipani, hali yangu taabani. Marehemu wangu baba, urithi kanitengea, Urithi mwingi si haba, ndugu wakajigawia, Na kwa upanga wa shaba, mbio wakanitimua, Nala nanywa mapipani, hali yangu taabani.

Uhakiki wa Maudhui ya Shairi

Dhamira

  • Dhuluma: Shairi linaonyesha jinsi ndugu wanavyoweza kumdhulumu mwenzao kwa kunyimwa urithi, hali inayopelekea maisha ya mateso.
  • Kutoa msaada: Jamii inahimizwa kusaidia waliodhulumiwa ili kudumisha upendo.
  • Elimu: Shairi linaonyesha umuhimu wa elimu katika kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Migogoro

  • Mgogoro kati ya ndugu na yatima anayenyimwa haki ya urithi wake.

Ujumbe

  • Mtu anapaswa kutafuta msaada badala ya kukaa kimya ili kupata haki yake.

Falsafa

  • Kupitia umoja na msaada wa jamii, haki inaweza kupatikana kwa walioonewa.

SHAIRI LA KISASA

Wanawake wa Afrika, Wakati wenu umefika, Unganeni, Shikaneni, Mjitoe utumwani, Nguvu moja. Nje kumepambazuka, Anzeni kukusanyika, Amkeni vitandani, Mtoke usingizini, Kumekucha. Tamkeni hadharani, Yote yanayowakera, Si mababu, Mhutubu, Kutetea haki zenu, Msichoke.

Uhakiki wa Maudhui ya Shairi

Dhamira

  • Ukombozi wa Mwanamke: Shairi linahimiza wanawake kujikomboa kutoka kwenye ukandamizaji wa kijamii na kiutamaduni.
  • Elimu: Shairi linahimiza wanawake kupata elimu kama njia ya kujikomboa.
  • Ushirikiano: Linasisitiza mshikamano miongoni mwa wanawake kama njia ya kufanikisha ukombozi wao.
  • Ujasiri: Mwanamke anapaswa kuwa jasiri na kujitokeza kutetea haki zake.

Ujumbe

  • Mwanamke anapaswa kuwa na ujasiri wa kujikomboa na kutafuta nafasi sawa na wanaume.

Falsafa

  • Kupitia mshikamano, wanawake wanaweza kujikomboa na kushika nafasi za uongozi.

Msimamo

  • Mshairi ana msimamo wa kimapinduzi, akihamasisha wanawake kujitokeza na kudai haki zao.

Mtaazamo

  • Mshairi ana mtazamo wa kiyakinifu, akihimiza wanawake kuchukua hatua badala ya kungoja mabadiliko yawepo bila juhudi zao.

Swali

Mashairi ya kisasa hayatumii vipengele gani kujenga mdundo wa kishairi?

Ingia ili kuwasilisha jibu lako na lihesabiwe katika umahiri wako.

Ingia ili kufanya mazoezi

Mwalimu

Umekwama? Niulize chochote kuhusu mada hii.

Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu swali hili.

Ingia ili kuuliza