Mada za sehemu hiiKumudu chimbuko la ukoloni mamboleoMada 3
- Kueleza dhana na chimbuko la ukoloni mamboleo
- Kuchambua athari za ukoloni mamboleo kwa Tanzania kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kimaadili
- Kutathmini mikakati ya kitaifa katika kupambana na ukoloni mamboleo
Ukoloni mamboleo ni hali ambayo, licha ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi zilizokuwa makoloni zinaendelea kudhibitiwa na mataifa ya kigeni kwa njia zisizo za moja kwa moja. Katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 1966, Tanzania ilijikuta ikikabiliana na changamoto hizi baada ya kupata uhuru.
Ukoloni mamboleo ni mfumo ambao mataifa ya kibeberu, pamoja na mashirika na taasisi za kimataifa, huingilia na kudhibiti mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya mataifa yaliyokuwa makoloni kwa madhumuni ya kuendelea kunyonya rasilimali za mataifa hayo. Hii hufanyika bila kuwepo kwa wakoloni moja kwa moja, lakini athari zake huendelea kuonekana katika nyanja mbalimbali.
Osagyefo Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana, alieleza ukoloni mamboleo kama hali ambayo "serikali ambayo inaonekana kuwa huru kwa mujibu wa sheria na kwa kuonekana kuwa na bendera na sifa zote za uhuru wa kimataifa, kwa hakika mfumo wake wa uchumi, na hivyo sera zake za kisiasa, hudhibitiwa kutoka nje."
Mwl. Julius K. Nyerere alibainisha kuwa hata baada ya uhuru, mataifa ya Afrika yaliendelea kuwa tegemezi kiuchumi, kijeshi na kisiasa, hali iliyokwamisha juhudi za ukombozi kamili wa Bara la Afrika.
Ukoloni mamboleo una sifa kuu zinazoweza kugawanyika katika vipengele vifuatavyo:
1. Utegemezi wa Kiuchumi
Nchi zilizokuwa makoloni ziliendelea kuwa tegemezi kiuchumi kwa mataifa yenye nguvu kutokana na muundo wa uchumi wa kikoloni uliowekwa kabla ya uhuru. Wakati wa ukoloni, nchi hizi zililazimika kuzalisha malighafi kwa ajili ya mataifa ya viwanda vya Ulaya Magharibi, huku zikiwa na uwezo mdogo wa kuzalisha bidhaa za viwandani. Baada ya uhuru, utegemezi huo haukuisha.
Mfano: Tanzania ilikuwa inauza mazao kama pamba, kahawa na korosho kama malighafi, badala ya kuyasindika ndani ya nchi. Faida kubwa ikwenda kwa wawekezaji wa kigeni, wakati Tanzania ikabaki tegemezi.
2. Misaada na Mikopo
Nchi huendesha shughuli zake za kiuchumi kwa kutegemea misaada au mikopo kutoka mataifa tajiri au taasisi za kifedha za kimataifa kama Benki ya Dunia na IMF. Mara nyingi, masharti hayo yanalazimisha mabadiliko ya sera, uimarishaji wa taasisi, na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Masharti hayo yanaweza kujumuisha kupunguza matumizi ya serikali na kurekebisha bajeti.
3. Wageni kudhibiti Sekta Muhimu
Sekta muhimu kama vile mawasiliano, uchukuzi, madini na viwanda huwekwa chini ya udhibiti wa wawekezaji wa kigeni. Makampuni ya kimataifa ndizo humiliki na kuendesha shughuli kubwa za kiuchumi. Ingawa uwekezaji huo huchangia ukuaji wa uchumi, faida mara nyingi sio endelevu kwani wawekezaji huchukua sehemu kubwa ya mapato na kuyapeleka katika mataifa yao ya asili.
4. Mwingiliano wa Utamaduni
Kupitia elimu, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, filamu na muziki, mataifa makubwa huendeleza utawala wa kiutamaduni. Nguvu ya mawasiliano husambaza maadili, tabia na mitindo ya maisha ya mataifa hayo, hali inayosababisha jamii kuiga utamaduni wa kigeni na kuacha tamaduni zao za asili.
5. Kuingilia Kisiasa
Mataifa ya kibeberu huingilia mifumo ya kisiasa ya nchi maskinini kwa lengo la kulinda maslahi yao. Uingiliaji hufanyika kwa kuunga mkono viongozi wanaolinda maslahi ya mataifa hayo, na wakati mwingine kwa kuchochea mapinduzi ya kijeshi.
6. Ushirikiano wa Kijeshi
Baadhi ya mataifa yanayoendelea hutegemea mataifa ya kibeberu katika shughuli za kijeshi. Hali hii huwezesha mataifa ya kibeberu kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya kiulinzi na kiusalama.
Chimbuko la ukoloni mamboleo linahusu sababu zilizosababisha kuibuka kwa mfumo huu baada ya uhuru wa kisiasa. Sababu kuu ni:
1. Athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia
Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilikuwa na mchango mkubwa katika kuharakisha kuibuka kwa ukoloni mamboleo. Baada ya vita hiyo, nchi nyingi zilizokuwa makoloni zilianzisha harakati za kudai uhuru. Mataifa yaliyokuwa na makoloni kama Uingereza, Ufaransa na Ubelgiji yalidhoofika kiuchumi na kuweza kuendeleza utawala wa moja kwa moja.
Mwaka 1942, Marekani chini ya Rais Franklin D. Roosevelt iliingia Mkataba wa Atlantic Charter na Uingereza. Mkataba huo ulihimiza haki ya mataifa kujitawala na kuwalazimisha Uingereza kuyapa uhuru makoloni yake. Hata hivyo, mazingira yaliyotokana na vita hiyo yaliandaa msingi wa kuibuka kwa ukoloni mamboleo.
2. Kupatikana kwa Uhuru wa Kisiasa
Kupatikana kwa uhuru wa kisiasa katika miaka ya 1950 hadi 1970 kwa nchi nyingi za Afrika kulichangia kuibuka kwa ukoloni mamboleo. Ingawa nchi hizi zilipata uhuru rasmi na kukomesha utawala wa moja kwa moja wa kikoloni, zilibaki na miundo ya kiuchumi na kisiasa iliyokuwa imejengwa awali kwa manufaa ya mataifa ya Ulaya.
3. Kutegemea Uchumi wa Kikoloni
Wakati wa utawala wa kikoloni, watawala wa kuunda mifumo ya kiuchumi iliyojikita katika uzalishaji na usafirishaji wa malighafi kutoka makoloni kwenda mataifa ya viwanda. Baada ya uhuru, nchi nyingi zilirithi mifumo hiyo bila kufanya mabadiliko makubwa.
Mfano: Tanzania ilirithi mfumo wa kilimo cha biashara ambao ulikuwa na tija kwa wakoloni. Baada ya uhuru, mkakati huo haukubadilishwa kwa kiasi kikubwa, na nchi iliendelea kutegemea masoko, teknolojia na mitaji kutoka nchi za Magharibi.
4. Masharti ya Kifedha na Mikopo
Mikopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia yamekuwa nyenzo muhimu za udhibiti wa kiuchumi. Masharti magumu yamejumuisha kupunguza matumizi ya serikali katika huduma za jamii, kuongeza mifumo ya kodi, kutoa vikwazo vya kibiashara, na kufungua milango kwa wawekezaji wa kigeni.
Matokeo yake, serikani nyingi zililazimika kutekeleza sera ambazo hazikuwa chaguo lao la msingi bali zilithiriwa au kuamuliwa na taasisi za kifedha za kimataifa. Hii ilisababisha utegemezi wa kudumu wa kifedha.
Kwa kutumia nadharia ya Kwame Nkrumah, tunaweza kuelezea jinsi ukoloni mamboleo unavyoendelea kuathiri maendeleo ya Tanzania. Kwa mfano, licha ya kupata uhuru wa kisiasa mwaka 1961, Tanzania iliendelea kutegemea Benki ya Dunia na wahisani wa kigeni katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Masharti ya mikopo hiyo yalilazimisha serikali kufuata sera zinazolinda maslahi ya mataifa yenye nguvu, badala ya kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi wa Tanzania.
Ukoloni mamboleo unaweza kueleweka katika maisha ya kila siku kwa mtanzania. Kwa mfano, unaponunua simu ya rununu au vifaa vya Umeme vyenye bei nafuu vya Kichina au ya Kihindi sokoni, unajionea kuwa uchumi wa nchi yetu bado unategemea bidhaa za nje. Hali hii inalingana na dhana ya ukoloni mamboleo ambapo nchi yetu inaendelea kuwa tegemezi katika uzalishaji wa bidhaa, badala ya kuzalisha vifaa hivyo ndani ya nchi yetu wenyewe. Pamoja na hayo, mikopo ya kigeni inayotumika kujenga barabara na miundombinu nyingine inakuja na masharti ambayo huathiri sera za serikali, na hatimaye maisha ya kila mtanzania.
Swali
Ukoloni mamboleo ni hali ambayo, licha ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi zilizokuwa makoloni zinaendelea kudhibitiwa na mataifa ya kigeni kwa njia zisizo za moja kwa moja. Hali hii inalingana na maelezo gani kati ya yafuatayo?
Ingia ili kuwasilisha jibu lako na lihesabiwe katika umahiri wako.
Ingia ili kufanya mazoeziMwalimu
Umekwama? Niulize chochote kuhusu mada hii.
Ingia ili kumuuliza Mwalimu wa AI wa Sonza kuhusu swali hili.
Ingia ili kuuliza